Umasikini wapungua Zanzibar
Huduma za jamii zapatikana bila usumbufu
NA MWANTANGA AME
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, tangu iliingia madarakani Novemba 3, mwaka 2010 na ifikipo mwezi Oktoba itakuwa ndio inafikia ukomo wake, kwa vile serikali itaitisha uchaguzi Mkuu.
Uchaguzi huo, utafayika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Katiba ya Zanzibar, ambayo inataka kila aliyepewa jukumu la kuiongoza nchi anapofikia miaka mitano basi uitishwe uchaguzi Mkuu.
Hadi hivi sasa Chama kinachoongoza nchi hii ni Chama cha Mapinduzi, ambacho kwa kiasi kikubwa kimeweza kudumu kwa miaka mingi tangu yafanyike Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, 1964.
Huu ni mwezi Septemba ni takriban miaka 10 tokea Novemba 2010, ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein alipata kwa mara ya kwanza, imani na ridhaa ya Wazanzibari ya kuwa mkuu wa nchi yao ya Zanzibar, akiwa ni Rais wao.
Aidha, hiki ni kipindi chake cha pili tokea mwaka 2016, baada ya kuchaguliwa na wananchi kufuatia ridhaa ya Chama kilichoongoza nchi hii kwa zaidi ya miaka 40 sasa, ambapo Chama cha Mapinduzi, kimekaa madarakani.
Ukichanganya na kipindi kilichoongozwa na mojawapo ya Chama kiasisi kwa CCM, Chama cha Afro Shirazi, cha kuanzia Januari 12, 1964, vyama hivi vya Ukombozi na Mapinduzi vimeshaongoza nchi kwa uweledi na mafanikio makubwa kwa miaka 56 sasa.
Kuwepo madarakani chama hiki ni sehemu ya kupima uwezo wake wa kuongoza katika njia zinazofaa za kuwatumikia wananchi kwa kila aliyepewa dhamana.
Kutokana na hali hiyo ndio maana chama cha Mapinduzi kimeamua kuweka ilani ya CCM ambayo inakuwa ni muongozo mzuri kwa aliyepewa jukumu la kuiongoza nchi kuutumia kufanya shughuli zake.
Moja ya jambo ambalo limo katika utekelezaji wa ilani hiyo ni suala la Kupambana na Umasikini, ikiwa ni kifungu cha 70 cha Ilani hiyo ambapo kinaelekeza mabo mbali mbali kufanyika ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba.
Ndani ya miaka mitano ya mwanzo ya uongozi wa Dk. Shein, umeeleza kwamba, Ili kuongeza nguvu na kasi ya kupambana na umasikini katika kipindi kilichopita (2010-2015), Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi umeanzishwa.
Kwa kupitia mfuko huo wananchi wengi hususan vijana, wanawake na wafanyabishara wadogo wadogo wameweza kupatiwa mitaji (mikopo) na kujikwamua kiuchumi.
Kutokana na muongozo huo wa ilani, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, kwa kipindi cha miaka 10 ndie aliyepewa jukumu na wananchi la kusimamia utekelezaji wake mambo hayo katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Tangu aingie madarakani Dk. Shein, kuna mambo mengi imeonekana kayatekeleza kwa kila mwaka wake aliyokuwepo kupitia sekta mbali mbali huku akiongozwa na malengo ya serikali ya Milenia Vison 2020.
Mbali ya utekelezaji wa será hiyo pia, Dk. Shein katika utawala wake huo alilazimika kufuata Mpango Mkuu wa kupambana na Umasikini wa MKUZA, ambao sasa upo katika awamu ya tatu sasa.
Aidha mafanikio yaliopatikana yametokana na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika kipindi cha 2010 – 2015 na 2015 – 2020.
Ilani hiyo imeweka dira imara ambapo Dk. Ali Mohamed Shein, amekuwa kinara wa kusimamia pamoja utekelezaji wa mpango wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini (MKUZA), uliokwenda sambamba na utekelezaji wa malengo ya Jumuiya ya MDGs na kimataifa ya SDGs.
Miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyosajiliwa Zanzibar kuanzia mwaka 2010 hadi sasa ni pamoja na Kuzidi kupungua hali ya umaskini nchini.
Hii ni utokana na taarifa za awali za matokeo ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya wa mwaka 2019, zinaonesha kuwa kwa ujumla, idadi ya watu wanaoishi katika umaskini wa mahitaji ya lazima (basic needs poverty) imepungua.
Hali hiyo, imepungua kutoka asilimia 30.4 mwaka 2014 hadi asilimia 25.7 mwaka 2019, wakati watu wanaoishi katika umaskini wa chakula (food poverty) wamepungua kutoka asilimia 10.8. hadi 9.3 katika kipindi hicho.
Kuimarika kwa mapato ya ndani ya Serikali kutoka shilingi bilioni 221.7 mwaka 2010/2011 hadi shilingi bilioni 741.2 bilioni mwaka 2018/2019 kimetajwa ndio chanzo cha kupungua kwa hai ya umasikini katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Mafanikio hayo yalikwenda sambamba na kuimarika kwa kujitegemea kufuatia kupungua sana utegemezi wa Bajeti kutoka asilimia 30.2 mwaka 2010/2011 hadi asilimia 5.1 mwaka 2018/2019 kwani awamu ya saba imeongeza Bajeti yake kwa mara 3.2 kutoka shilingi bilioni 444.6 mwaka 2010/2011 hadi shilingi trilioni 1.4 mwaka 2019/2020.
Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Mohamed Ramia, akitoa tarifa ya hali ya umasikini kwa kipindi cha miaka 10, alisema imeimarika na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2020 imeonekana imekamilika kwa mafanikio makubwa.
“Ni matumaini yetu kwamba utekelezaji wa Dira mpya ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050 utaanza kwa muda uliopangwa na kumuachia mrithi wa uraisi atakayechaguliwa kuendeleza miongozo na mikakati imara ya kuitekeleza Dira hiyo kwa miaka 10 ya mwanzo, ili kuleta maendeleo kwa Wazanzibari wote” alisema.
Alisema utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2020 na mipango ya muda wa kati iliweka misingi imara kwa wadau wote.
“Sisi sote ni mashahidi wa mafanikio yaliyopatikana katika vipindi tofauti, kupungua kwa umasikini uliokithiri na kufikia asilimia 10.8 kwa mwaka 2014/15 na kukaribia lengo la Dira la asilimia 10 lililowekwa kufikia mwaka 2020”, alisema.
Alisema katika kupunguza idadi ya kaya masikini, Serikali imewapatia misaada ya kifedha na kitaaluma, ili kuanzisha miradi itakayowapatia kipato chao na kujitegemea.
Alisema taarifa ya awali ya utafiti wa mapato na matumizi ya Kaya ya mwaka 2019/2020, inaonesha kuwa umaskini umepungua zaidi na kufikia asilimia 9.3.
Sambamba na hilo, alisema Zanzibar imefikia Hadhi ya nchi zenye Uchumi wa Kipato cha Kati, ikiwa na Pato la Taifa la Dola za Kimarekani 1,114 kwa kila mtu mwaka 2019, ambapo kiwango cha hadhi ya nchi hizo huanzia Dola za Kimarekani 1,026.
Aidha alisema umri wa kuishi kwa Wazanzibari umeongezeka kutoka miaka 48 mwaka 2000, na kufikia miaka 65 mwaka 2012.
Naye, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, ambaye Ofisi yake inasimamia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF, ikiwa ni sehemu ya kupambana na umasikini alisema hali ya umasikini Zanzibar imepungua.
Alisema serikali ndani ya kipindi cha miaka 10 ya Urais wa Dk. Ali Mohamed Shein, imeratibu utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF III) uliotekelezwa katika Shehia 204 (Unguja 126 na Pemba 78) ambapo katika kipindi hiki shughuli kadhaa zimetekelezwa katika Mpango huo.
Aliyataja mambo hayo alisema ni pamoja na Malipo kwa kaya masikini 31,870 (Unguja 17,801 na Pemba 14,069) kutoka Shehia 204 yametolewa ambapo Jumla ya Shilingi 1,164,540,000 zimelipwa kwa kaya 31,870.
Alisema Mafunzo ya uandaji wa mipango rahisi ya biashara yametolewa katika Shehia zote 204 za Mpango wa kupambana na umasikini Unguja na Pemba, ambapo jumla ya Shilingi 271,700,000 zilitumika.
Alifahamisha kuwa mafunzo hayo yamewawezesha walengwa wote kubuni na kuandaa mipango ya biashara mbalimbali na tayari imeshawasilishwa.
Akitaja mambo mengine ambayo serilai imeyasimamia ndani ya miaka hiyo 10 ni pamoja na kusimamia na kufuatilia shughuli za uhamasishaji walengwa juu ya kuweka akiba na kukuza uchumi wa kaya zao kupitia vikundi vya Kuweka Akiba na Kukuza Uchumi wa kaya.
Alisema jumla ya Shilingi Bilioni 2.1 zimewekwa katika vikundi 2,047 Unguja na Pemba, na Ujenzi wa kituo cha Afya na utiaji wa samani na vifaa husika ambao uligharimu Shilingi 164,000,000 katika Shehia ya Kianga, Wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja umekamilika na Kituo hicho tayari kimeanza kutoa huduma.
Alisema kazi hiyo imefikia asilimia 100 ya lengo la Dira; na Uandikishaji wa wanafunzi kwa elimu ya msingi umefikia asilimia 118.1 mwaka 2019 zaidi ya lengo la Dira la asilimia 100.
Huduma za ustawi wa jamii kwa wazee na watoto zimeendelezwa kwa kuwapatia makaazi mazuri yenye usalama, huduma za chakula na matibabu na watu wenye ulemavu wamepatiwa zana na vifaa vinavyowasaidia katika suala la elimu na ajira; Uchumi wa Zanzibar umefikia asilimia 7.0 mwaka 2019 badala ya asilimia 8-10 iliyopangwa kufikiwa na Dira.
Haya ni mafanikio ya zaidi ya asilimia 70; Kufuatia kukamilika kwa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2020, na sasa Serikali iko katika hatua za uandaaji wa Dira mpya ya Maendeleo ya mwaka 2050 ambapo rasimu ya awali imekamilika, ikiwa ni hatua itayosadia zaidi kupunguza umasikini na uchumi kuimarika.
Mwelekeo wa Dira hiyo unajikita katika kufanya mageuzi ya uendelezaji wa sekta za ukuzaji uchumi zikiwemo kilimo, utalii na viwanda na sekta za kijamii zikiwemo, elimu, afya na maji, ili kufikia malengo yaliyowekwa na Dira ya Maendeleo ya 2050.
Alisema hivi sasa sekta za Uchumi wa Buluu, Mafuta na Gesi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ili ziweze kuchangia harakati za ukuzaji uchumi na uimarishaji wa ustawi wa jamii.