Sekta ya elimu Pemba ya kupigiwa mfano

Visiwa vidogo vyote vyapata skuli

Wananchi wammiminia shukrani rais

NA HANIFA SALIM, PEMBA

IKIWA Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametimiza miaka 10 ya uongozi wake tangu aingie madarakani mwaka 2010 wananchi wa Pemba wanajivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana kipindi hiki cha uongozi wake.

Ni dhahiri Dk. Shein ni kiongozi jasiri, mweledi, mwenye fikra sahihi za kuwaletea wananchi wa Zanzibar maendeleo, kupitia Sekta mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika kuhakikisha Zanzibar inakuwa na maendeleo Dk. Shein amesimamia vilivyo utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambacho kilimpa tiketi ya kuwania urais kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano.

Katika makala hii maalumu tunazungumzia Sekta ya elimu iliyopiga hatua kubwa ndani ya kisiwa cha Pemba ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake.

Kwa mujibu wa hotuba yake Rais Dk. Shein wakati akilivunja Baraza la tisa la Wawakilishi Zanzibar Juni 20/2020, alisema ni jambo la kufurahisha, kuona mafanikio makubwa ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeyapata.

Alisema, katika utekelezaji wa malengo iliyojiwekea upande wa Sekta ya Elimu, ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2010-2015, Ilani ya mwaka 2015-2020, Dira ya Maendeleo ya 2020 na Mipango mingine ya Kitaifa.

Alisema, “wakati tukiwa katika mwaka wa 10 wa uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tunafarajika kwa mafanikio makubwa ya kuandikisha watoto wote waliofikia umri wa kusoma”.  

Serikali imeondoa michango ya wazazi katika elimu ya msingi katika mwaka 2015/2016 na kuondoa gharama za mitihani ya skuli za sekondari kuanzia mwaka fedha 2016/2017, ili kuwawezesha watoto wote wapate elimu bure kwa shabaha ya tamko la mwasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, alilolitangaza Septemba 23 mwaka 1964.

Katika kipindi hiki cha miaka 10, Serikali ya Mapinduzi imeongeza idadi ya wanafunzi wapya wanaoandikishwa katika ngazi ya elimu ya lazima ya Maandalizi, Msingi na Sekondari kutoka jumla ya wanafunzi 317,278 mwaka 2010 hadi kufikia wanafunzi 529,688 mwaka 2020.

Aidha alisema Skuli za msingi zimeongezeka na zimefikia skuli 381 zenye wanafunzi 290,510 mwaka 2019, kutoka skuli 299, zilizokuwa na wanafunzi 226,812 katika mwaka 2010, ogezeko la skuli ni asilimia 27.4 na ongezeko la wanafunzi ni asilimia 28.

Kwa upande wa skuli za sekondari, hivi sasa zipo skuli 287 zenye wanafunzi 135,519, ikilinganishwa na skuli 105, zilizokuwa na wanafunzi 80,008, katika mwaka 2010.

“Ongezeko la skuli ni asilimia 73.3 na ongezeko la wanafunzi ni asilimia 69.4 ambapo majengo kadhaa ya ghorofa ya skuli za Msingi na Sekondari yamejengwa na Serikali katika Wilaya zote za Unguja na Pemba”, alisema. 

Vile vile, Serikali imejenga vituo 22 vya ubunifu wa kisayansi (13 Unguja na 9 Pemba) ambavyo kwa jina la kitaalamu vinaitwa “Hubs” vituo hivyo vyenye maabara za sayansi, vyumba vya kompyuta, maabara za lugha, maktaba na vyumba vya kujisomea wanafunzi.

“Mafanikio yote yaliyopatikana yametokana na kuongezeka bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imeongezwa mara 3.8 kutoka shilingi Bilioni 47.093 mwaka 2010/2011 na kufikia shilingi Bilioni 178.917 mwaka 2019/2020”, alisema.

Naye Ofisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba, Mohamed Nassor Salim alisema, mradi wa skuli mpya ni miongoni wa skuli ambazo zinajengwa kupitia mradi wa ZISP katika visiwa vidogo vidogo ndani ya Kisiwa hicho.

Anaeleza katika awamu ya saba ya Serikali ya Zanzibar inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein imefanikiwa kutekeleza kifungu cha 100 cha Ilani ya chama cha Mapinduzi kinachoeleza ahadi ya chama kwa wananchi.

“Rais wetu wa awamu ya saba amemudu katika kipindi chake cha miaka 10 kwanza kuhakikisha kila kisiwa kinachoishi wananchi wake kusini na kaskazini ya Pemba kinapata huduma za elimu bora”, alisema.

Aliongeza kuwa visiwa vidogo vidogo vilivyopo ndani ya Pemba ambavyo ni kisiwa Panza, Makoongwe, Kojani, Uvinje, Kokota, Fundo na Njau visiwa hivi vyote saba kwa sasa huduma ya elimu inapatikana.

Alifahamisha kuwa, kuenea kwa skuli katika visiwa vyote hivyo ni mafanikio nambari moja, utanuzi wa huduma ya elimu kutoka ngazi ya msingi hadi Sekondari kwa visiwa vinne kati ya visiwa saba vilivyopo Pemba.

“Ndani ya miaka 10 hii ya Serikali ya awamu ya saba Kojani, Kisiwa Panza, Makoongwe na Fundo kwa sasa vina elimu ya Sekondari hili ni jambo la kujivunia katika utawala wa Dk. Shein”, anaeleza.

Anasema, visiwa vitatu kati ya visiwa vinne ambavyo zimejengwa skuli za Sekondari kuboreshwa vyumba vya masomo ya lugha hasa kiingereza, chumba cha kompyuta na maabara za sayansi.

Anaeleza, kuenea kwa vifaa vya kisasa kutapelekea elimu kuwa bora zaidi katika visiwa vidogo vidogo, huku kupitia agizo la Rais la kuajiri walimu kwa sasa vibali 12 vimeshatolewa kwa ajili ya skuli ya sekondari Kojani tu ili kutoa elimu bora zaidi.

“Walimu hao wanatoka ndani ya kisiwa cha Kojani kwenyewe kwani lengo la kufanya hivyo ni kufanya ushindani wa vijana kusoma na kupata kazi lakini pia kupata walimu ndani ya kojani kutarahisisha utoaji wa elimu kwa muda muafaka”, alisema.

Alifahamisha, jamii ya visiwani imehamasika kwa uandikishaji mkubwa wa wanafunzi hata ufaulu umeongezeka hatua kwa hatua ukiangalia mwaka 2010 hadi 2020.    

Afisa mdhamini huyo aliongeza kuwa skuli hizo zimezingatia mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu, ambapo chini zina vyumba vya maabara, maktaba pamoja na Vyumba vya Kompyuta na juu ni madarasa ya kusomea wanafunzi.

Alieleza kuwa, dhamira ya ujenzi wa skuli hizo ni kuona wanafunzi wa visiwa vidogo vidogo wanapata elimu bora, kushindana kimasomo na katika soko la ajira kama wanafunzi wa maeneo mengine ya Visiwa vya Zanzibar.

“Ujenzi wa Visiwani una changamoto nyingi ikiwemo za kimazingira kama vile usafirishaji wa vifaa vya ujenzi lakini watendaji wetu wamefanya jitihada kubwa katika kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa muda muafaka”, alisema.

“Zaidi ya shilingi bilioni moja zimetumika kukamilisha ujenzi wa skuli ya sekondari ya Kojani ambayo inajengwa kupitia mradi wa ZISP huku ujenzi wa skuli za Fundo, KisiwaPanza na Makoongwe zikiwa na thamani zaidi ya shilingi milioni 27,000,000.

Kwa upande wake meneja msimamizi wa ujenzi wa skuli ya sekondari Kojani kutoka kampuni ya Home Afrika, Richard Charo alisema, mradi huo umeanza mwaka 2018 na kutarajia kumalizika Machi mwaka huu lakini kutokana na changamoto za usafirishaji wa vifaa umechelewa.

“Kama tunavyojua ni Kisiwa na Visiwani kuna changamoto ya usafiri kama ingelikua ni kama sehemu nyengine zenye barabara ujenzi huu tayari ungekamilika mapema zaidi”, alisema.

Mwalimu Mkuu wa skuli ya sekondari Kojani, Bakar Issa Omar alisema, skuli hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri na yenye ubora wa kielimu itakapokamilika.

“Tunaishukuru sana Serikali kwa kuona ipo haja kutupatia skuli yenye mazingira mazuri ya kusomea hapa tuna vyumba vya kompyuta na Maabara za Kisayansi naamini wanafunzi watasoma kwa bidii zaidi”, alisema.

Mwananchi wa Kisiwa cha Kojani, Khamis Amour Khamis alisema, ujenzi wa skuli hiyo ya kisasa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM hivyo watafarijika zaidi kuona skuli hiyo inapatiwa walimu watakaowawezesha wanafunzi kuingia katika ushindani wa kimasomo.

Alisema kuwa, wananchi wa Kojani matumaini yao skuli hiyo itakuwa ni miongoni mwa skuli kubwa za kupigiwa mfano zenye kutoa elimu bora kwa wanafunzi kama vile Fidel Castro, Madungu, Mitiulaya na Utaani kwa Kisiwa cha Pemba.

“Tunamuomba Rais wetu wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein skuli yetu itakapomalizika kuja kutufungulia kwani tuna mengi ya kumpongeza wananchi wake hivyo ujio wake wananchi wa Kojani tutafarijika”, alisema.

Kibuyu Mjaka Haji mkaazi wa Kojani, alisema katika Kipindi cha miaka ya nyuma Kojani haijawahi kupatiwa maendeleo ya elimu kama ambayo yamepelekwa na Dk. Shein ndani ya uongozi wake wa miaka 10 wanafunzi wa Kisiwa hicho walilazimika kutoka nje ya Kisiwa kutafuta elimu ya juu baada ya kumaliza masomo yao ya kidato cha nne.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya skuli ya sekondari Kojani, Mize Hassan Iddi alisema, jamii ya Kisiwa hicho imefurahi vya kutosha kujengewa skuli ya kisasa na ambayo wananchi wanategemea kupokea elimu bora kwa wanafunzi.

Hata hivyo aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwapatia maendeleo katika sekta mama ya elimu na kumuomba Rais wa Zanzibar kushiriki kuwafungulia jengo hilo wakati litakapomalizika. 

Zakia Bakar Khamis mkaazi wa Kisiwa cha Makoongwe alisema, Dk. Shein ni rais wa kupigiwa mfano kulingana na maendeleo bora ambayo amekua akiwapatia wananchi wake na kuwajali kwa kuwaondoshea kilio walichokua nacho kwa miaka yote hapo awali.

“Tunamshukuru Dk. Shein kutupatia Skuli ya Sekondari ndani ya Makoongwe watoto wetu katika miaka yote iliyopita wanapomaliza masoma yao ya kidato cha nne wanalazimika kwenda nje ya Kisiwa kuendelea na masomo hili ni jambo kubwa na la kupigiwa mfano kiongozi wetu huyu”, alisema.  

Aliiomba wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali katika upangaji wa walimu watakaofundisha katika skuli za visiwani kuhakikisha wanakaa ndani ya visiwa hivyo ili wanafunzi wapate elimu kwa muda wote na sio kukosekana wanafunzi kupatiwa mafunzo kwa kisingizio cha kukosa walimu.

Asha Zubeir Haji mkaazi wa Kisiwa Panza yeye aliipongeza Serikali ya awamu ya saba inayoongozwa na Dk. Shein na alisema haikubakisha ahadi ambazo alizitoa kwa wananchi kwani imetekeleza kwa vitendo na hakuna wa kupinga suala hilo.

Alifahamisha, mafanikio mbali mbali yameonekana katika utawala wa Serikali hiyo kwani imeweza kuboresha sekta ya elimu katika visiwa vidogo vidogo kujenga skuli zenye vifaa na walimu bora watakaotoa elimu ndani ya visiwa hivyo.

“Ni mengi aliyotufanyia Dk. Shein katika Uongozi wake wa Serikali hii kwa muda wa miaka kumi na tutaendelea kumkumbuka milele kwani amefanya kazi kubwa ya kutuletea maendeleo wananchi wake bila ya ubaguzi wa aina yoyote ile,” alisema.

Wananchi hao wamemuombea Dk. Shein apumzike kwa amani huku akijua kuwa bado Wazanzibari wanahitaji busara na hekma zake wakati akistaafu.