Ilani ya CCM imetekelezeka vyema

Nyumba za makaazi zajengwa

NA MWANAJUMA MMANGA

UONGOZI imara wa serikali ya awamu ya saba chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, imepiga hatua kubwa na hakika ni ya kupigiwa mfano katika juhudi za kuwaletea maendeleo wananchi.

Katika kipindi cha miaka 10 ambacho muda si mrefu anategemewa kukamilisha muda wake wa uongozi, Rais Shein ameimarisha huduma za makaazi na kupatikana mafanikio mengi ya makaazi kwa wanaanchi.

Makala haya maalumu itaelezea namna ya nyumba za makaazi zinazomilikiwa na shirika la nyumba chini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zilizoko maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la nyumba Riziki Salum, aliliambia gazeti hili kuwa nyumba za makaazi ni moja ya vyanzo vya mapato kwa kuwa kodi itokanayo na nyumba hizo zinaingia serikalini moja kwa moja.

Katika kutekeleza sera ya Taifa ya nyumba, sheria No. 6 ya kuanzishwa Shirika la Nyumba la Zanzibar ya mwaka 2014, imepitishwa ili kuwapa fursa wananchi waliopangishwa nyumba za maendeleo Mjini na vijijini kuuziwa sehemu ya majengo hayo.

Aidha katika kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010-2020 imetekeleza na kusimamia maendeleo ya nyumba za makaazi kwa wananchi wa Unguja na Pemba, huku akiwa katika uongozi wake shirika hilo lilianzishwa ambapo hadi sasa linaendelea na utekelezaji wake vizuri.

Akitaja baadhi ya malengo mahasusi ya shirika hilo, mkurugenzi huyo alisema ni pamoja na kuimarisha uwezo wa Shirika katika kutoa huduma bora kwa wateja kwa kuwapatia nyumba bora za makaazi na uwekezaji.

Aliyataja malengo mengine ni kuimarisha majengo na miundombinu ya Shirika ili kuzitambua nyumba hizo, kuzisimamia na kuziendeleza.

MAFANIKIO

Kuhusiana na mafanikio ya Shirika, mkurugenzi huyo alisema kuanzia Julai 2015 hadi Juni 2020 shirika lilifanikiwa kufanya matengenezo ya nyumba 26 za Madungu Chakechake Pemba.

“Tunaendelea na matengenezo mengine ya nyumba 36 za maendeleo Michenzani kwenye nyumba nambari 1 ngazi ya kwanza pia tunazikarabati nyumba za shirika zilizoko Gizenga, Mazizini, Machomane, Malindi, Hurumzi, Kikwajuni na Kiponda”, alisema

Aidha mkurugenzi huyo alizitaja nyumba nyengine zinazoendelea na matengenezo kwa upande wa Pemba ni pamoja na nyumba za Selemu zilizopo Wete, Micheweni na Chakechake.

Mafanikio mengine ni pamoja na kuzibua na kusafisha mifumo ya maji machafu kwa nyumba kadhaa za Unguja na Pemba ambazo zinamilikwa na shirika hilo.

Mkurugenzi alitaja mambo mengine yaliyoimarishwa ni kuwekwa vibati vya nambari za utambuzi kwa nyumba za Mji Mkongwe kwenye mitaa ya Shangani, Forodhani, Gizenga, Kiponda, Mkunazini na Hurumzi. kazi hiyo inaendelea kwa mitaa mingine ya mji mkongwe iliyobaki.

“Shirika limehamasisha wapangaji kulipa kodi na kutunza nyumba za shirika kama kutoa elimu kupitia vipindi vya redio, televisheni, magazeti na kufanya mikutano na wakaazi wa nyumba za Michenzani, Kikwajuni, Gamba na Makunduchi”, alisema.  

Sambamba na hilo, lakini alisema serikali kupitia shirika la nyumba limetoa mikataba mipya ya ukodishaji nyumba kwa kupitia akaunti ya benki ya watu wa Zanzibar (PBZ).

“Kipindi cha uongozi wa awamu ya saba ya Dk. Ali Mohamed Shein, amekamilisha ujenzi wa nyumba za fleti za Mpapa huko Bambi wilaya ya kati Unguja ambapo jumla ya nyumba 24 zimeshapewa wananchi.

“Pamoja na kuzifanyia matengenezo ya nyumba kadhaa za maendeleo za Mtemani zilizopo Wete na za Madungu Chake chake Pemba ambapo hapo kabla nyumba hizo zilikuwa katika hali mbaya”, aliongeza.

Mkurugenzi huyo alisema katika uongozi huo wa Dk. Shein serikali pia imelifanyia matengenezo makubwa ya jengo maarufu la treni lililopo Darajani “Chawl” lililojengwa mwaka 1880 ili kulipa haiba nzuri jengo ambalo kwa sasa linatumika kwa makaazi na biashara.

Akivunja Baraza la Tisa la Wawakilishi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa

Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, alisema amefanya maendeleo makubwa katika nyumba na hadi sasa jumla ya nyumba 200 zimejengwa pamoja. 

“Mradi mwengine wa nyumba za makaazi unaoendelea kutekelezwa huko Nyamanzi na Kampuni ya CPS, ambapo hadi mwaka huu wa 2020, jumla ya nyumba za makaazi 465 zimejengwa. Nyumba 169, miongoni mwao zimeshamalizika na 120 zimeshakabidhiwa kwa wenyewe waliozinunua na naamini miongoni mwa Wajumbe wa Baraza hili mtakuwemo, nakupongezeni sana, hatua za ujenzi wa nyumba nyengine zinaendelea”, alisema Rais Shein.

Alisema Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) imekamilisha ujenzi wa majengo 15 ya nyumba za kisasa za ghorofa 7 zenye jumla ya fleti 210 huko Mbweni, ambapo fleti 146 tayari zimeuzwa na zilizobakia zimo katika utaratibu wa kuuzwa.

Rais Shein, alisema hivi sasa, Mfuko huo unaendelea na ujenzi wa majengo mawili yenye fleti 28 na kuanza ujenzi wa sehemu za michezo na biashara kwenye eneo hilo.

“Hadi sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa nyumba za kisasa kwa ajili ya wananchi katika eneo la Kwahani, ambapo majengo matatu ya ghorofa sita yenye fleti 70, yanaendelea kujengwa na Kampuni inayojenga itaikabidhi Serikali katika mwezi wa Septemba, 2020.  Hatua hii ya ujenzi ni Awamu ya Kwanza, ambapo ujenzi huu utaendelea katika awamu mbali mbali hapo baadae, hadi nyumba zote zitakapokamilika kujengwa katika eneo hilo”, alisema Dk Shein wakati akivunja baraza la wawakilishi mwezi wa Juni.

UIMARISHAJI WA NG’AMBO TUITAKAYO

Kuhusu uimarishaji wa Ng’ambo tuitakayo ni mkakati wa Rais Dk. Shein, ambapo kabla ya kumaliza muda wake ni kubadilisha mitaa ya Ng’ambu kwa kujenga nyumba za kisasa zenye mandhari ya kuvutia.

Zanzibar bado kuna maeneo mengi yanayohitaji kuekezwa mjini na vijijini ikiwemo Kwahani, Kijangwani, Kwalimsha na Kariakoo na maeneo ya vijijini ni Mkokotoni, Chwaka na Tunguu.

Nae Mkurugenzi wa Mipango Mji na Vijiji, Dk. Muhammad Juma, aliiambia makala haya kuwa mpango huo umeanza ujenzi wa nyumba za maendeleo Kwahani na baadae kuendelea maeneo mengine hatua kwa hatua.

“Kunafuatia agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kubadilisha madhari ya ya Zanzibar na kuwa mji wa kisasa”, alisema.

Alisema ujenzi wa kitovu cha mji wa Zanzibar, sio suala la kukurupuka badala yake linahitaji utaalamu na kutumia mbinu za kisasa na ushirikishwaji wa fikra za wananchi hasa ikizingatiwa ni jambo la kitaifa.

Makazi ni miongoni mwa mahitaji muhimu anayopaswa mwanadamu kuyapata ikiwa ni pamoja na chakula na mavazi.

Kwa kuona umuhimu huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein amelitilia mkazo na amewahakikishia Wazanzibar kuwa anapoondoka madarakani tayari ameweza kutekeleza ahadi yake hiyo kwa asilimia kubwa.