Huduma za afya Pemba zaimarika

Ukarabati, vifaa tiba na wataalamu waongezeka

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WANANCHI wa Zanzibar wana kila sababu ya kumpongeza Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ambae anatimiza miaka 10 tangu aingie madarakani mwaka 2010.

Dk. Shein katika uongozi wake amekuwa akipigania vitu vingi ili kuleta maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar kupitia nyanja mbali mbali, ikiwemo huduma na matibabu bure kwenye hospitali na vituo vya Afya.

Hii ni dhahiri kuwa Dk. Shein ni kiongozi jasiri, mweledi, mwenye fikra sahihi za kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar pamoja na kujali afya zao.

Dk. Shein amesimamia vilivyo utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwa kutekeleza ahadi mbali mbali alizoahidi kwa wananchi wake, ikiwemo huduma za afya bila malipo.

Makala haya maalumu yanazungumzia jinsi huduma za afya kwa ujumla wake kisiwani Pemba zilivyotekelezwa katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wa Rais Shein.

“Katika Wizara yetu ya Afya, Dk. Shein ameyaahidi mengi katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake na asilimia 99 ameyatekeleza tunashukuru sana”, anasema daktari dhamana wa hospitali ya Chake Chake, Dk. Ali Omar Khalifa.

Anasema kuwa, uboreshwaji wa huduma za matibabu, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ni miongoni mwa ahadi zake, ambapo alizitimiza kwa moyo wa imani kabisa.

“Ametuletea maendeleo thabiti bila kujali rangi, kabila na hata itikadi za kisiasa, alihakikisha wananchi wote wenye uwezo na wasio na uwezo wanapata matibabu, huduma za afya bure”, anaeleza.

Katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake Dk. Shein amejitahidi kuyafanya yote hayo kuhakikisha wananchi wanapata huduma bila ya usumbufu.

Dk. Khalifa anafahamisha kuwa, Dk. Shein alitimiza ahadi ya matibabu bure kwa wananchi wa Zanzibar na kwa sasa wanafurahia huduma hiyo ambayo zamani haikuwepo.

“Tunamshukuru sana Rais wetu kwa kutekeleza ahadi hizi, kwani amesimamia vifaa tiba ikiwemo X-ray, Ultra sound na huduma nyengine kwa wananchi bila ya malipo, ambavyo vimeenezwa mahospitali yote ya Unguja na Pemba”, anaeleza.

Katika hatua nyengine Dk. Shein alisimamia upatikanaji wa kada mbali mbali za Afya ikiwemo kuongezewa wafanyakazi, wahudumu, madaktari na wauguzi, jambo ambalo limeleta faraja kwao na wananchi kwa ujumla.

Anaeleza kuwa, wakati akiwa makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Shein ndiye aliyetoa moyo wake na kusema Zanzibar ipate madaktari wa kutosha na ndipo alipounda Kamati ya kutathmini nini kifanyike.

“Dk. Shein alikwenda nchini Cuba kuonana na viongozi wa nchi hiyo ili kuandaa darasa la kusomesha wanafunzi wenye sifa Zanzibar, ambapo walikubali ombi hilo”, anaeleza.

Baada ya miaka saba wakapata madaktari 50 waliohitimu, ambao wanafanya kazi kwenye hospitali za Unguja na Pemba, jambo ambalo ni la kujivunia kwa wazanzibari wote, kwani Dk. Shein alipigania kwa nguvu zote kwa lengo la kupatiwa wananchi huduma bora.

Dk. Khalifa anaeleza kuwa, madaktari hao wapo Unguja na Pemba na wanafanya kazi kwa ufanisi na weledi kabisa na pia waliendelezwa kwa kupewa udhamini wa kuendelea na masomo yao katika nchi za nje.

“Yote hayo ni kuhakikisha wananchi wanapata matibabu kutoka kwa madaktari wazalendo na sio kutegemea madaktari kutoka nje, hili ni la kupongezwa Rais wetu mpendwa”, anaeleza.

Akizungumzia hospitali anayoisimamia ya Chake Chake, Dk. Khalifa anasema, imepata mafanikio makubwa kiasi ambacho wananchi wanatoka sehemu mbali mbali kufuata huduma hospitalini hapo.

Kila siku wananchi wanaongezeka kwa sababu wanajivunia huduma zilizopo katika hospitali hiyo, kwani Dk. Shein amejitahidi kuimarisha miundombinu ikiwemo kuongeza majengo katika hospitali hiyo.

“Alitoa agizo kwamba hospitali hiyo ijengwe, kwani eneo ni finyu na idadi ya wagonjwa inaongezeka kila siku, ndipo Kamati ya Baraza la Wawakilishi ikabariki ujenzi huo na kupitisha bajeti”, anafafanua.

Kwa sasa hospitali hiyo inafanyiwa ukarabati mkubwa wa majengo matatu ambayo ni wodi ya wanawake, wazazi na watoto, ujenzi huo wa ghorofa moja unategemea kumalizika baada ya mwaka mmoja na wananchi watapata huduma ya kutosha kabisa.

“Wodi ya wazazi na watoto ilikuwa na vitanda 27 kwa kila wodi moja, lakini baada ya ujenzi kukamilika wanatarajia kuchukua idadi kubwa ya wagonjwa wa maradhi mbali mbali, kwani vitanda vitaongezeka mara mbili zaidi”, anaeleza.

Alisema kuwa katika ujenzi huo kutakuwa na chumba cha ICU, vyumba vya dharura (emergency department), ghala ya kuhifadhia dawa na pia kutakuwa na nafasi ya kutosha kwa wagonjwa.

“Jengo hilo linatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 2.4 mpaka kumalizika kwake, hivyo Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alipambana kuhakikisha hospitali hiyo inakuwa imara na inahudumia watu wengi kwa wakati mmoja”, alisema.

Dk. Khalifa anataja kuwepo madaktari wasiopungua 10, wauguzi wasiopungua tisa na wahudumu wengi katika hospitali hiyo kiasi ambacho wagonjwa wanapata huduma ipasavyo bila ya kubahatisha.

Daktari huyo aliiomba jamii kuwa wastahamilivu katika kipindi hiki cha ujenzi wa hospitali hiyo, kwani alilolifanya Dk. Shein ni jambo kubwa na la mfano.

Pia aliwataka wazanzibari kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kushirikiana na viongozi katika kuiletea nchi maendeleo.

Kwa upande wa wananchi wanaokwenda hospitalini hapo kufuata huduma wameishukuru serikali ya Awamu ya saba chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa kuwapatia huduma za afya bure hasa kwa mama wajawazito.

“Miaka 10 ya uongozi wa rais wetu mpendwa Shein tumefaidika sana, ukienda hospitali unapata vipimo tena ni bure, tuinajivunia kwa kweli, Allah ampe kila lenye kheri”, wanasema.

Khamis Ali Hamad mkaazi wa Chake Chake, anasema katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake Rais Shein alifanya mambo mengi katika sekta ya afya ambayo wanajivunia.

“Zamani X-ray au Ultra sound unalipia ,lakini kwa sasa ni bure vipimo vyote tunashukuru sana”, anaeleza.

Mama mmoja ambae hakutaka jina lake litajwe anasema kuwa, huduma za mama na mtoto zimeimarika, ambapo wanajipatia matibabu bure.

“Kwa kweli ni faraja na furaha kwetu akina mama, maana tunapata matibabu bure tangu tukiwa na ujauzito mpaka na watoto wetu, hilo ni jambo kubwa alilotupatia Dk. Shein”, anafahamisha.

Kwa mukhtaza huo basi, kuna kila sababu ya kumpongeza Dk. Shein kwa mambo mengi aliyoyafanya kwenye sekta ya Afya katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wake hapa kisiwani Pemba.