Sekta misitu yaimarishwa

Doria zasaidia kupunguza uharibifu

NA TATU MAKAME

NI miaka 10 tangu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aingie madarakani kuongoza nchi hii ambapo mambo kadhaa ya huduma za kimaendeleo zimefanikiwa katika uongozi wake.

Katika utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) sambamba na utekelezaji wake wa ahadi za wananchi wakati akiomba ridhaa ya wananchi, Rais Shein daima atakuwa ni kioo wakati akimaliza muhala wake wa uongozi kipindi kifupi kijacho.

Miongoni mwa sekta ambazo amezitendea haki ni Idara ya Misitu na Maliasili zisizo rejesheka Zanzibar ikiwemo kupiga doria na uhifadhi wa wanyama ambao ni kivutio kikubwa cha utalii.

Akizungumza na mwandishi wa Makala haya, Ofisa Mkuu Idara ya Misitu Mali asili zisizorejesheka, Miza Suleman Khamis, alisema Idara hiyo imetekeleza mambo mbalimbali.

Miongoni mwa yaliyotekelezwa ni kupatikana kwa sera ya misitu na sheria ya uhifadhi na usimamizi wa rasilimali za misitu zenye lengo la kudhibiti na kuhifadhi mali zikiwemo raslimali za misitu, maliasili zisizorejesheka na wanyama pori.

Mambo mengine ni ushirikishwaji wa wananchi katika usimamizi na uhifadhi wa maeneo tengefu ya Jozani na Ngezi pamoja na misitu ya asili ya Masingini na Msitu Mkuu na Kiwengwa.

“Ushirikishwaji wa wananchi umefanyika katika utunzaji na uhifadhi wa wanyama adimu walio katika hatari ya kutoweka hususan kima Punju, Popo wa Pemba na Paa Nunga sambamba na kuyaimarisha maeneo mapya ya hifadhi ya kima Punju huko Muyuni.

Usimamizi wa mikataba 50 ya misitu ya jamii na matumizi endelevu ya maliasili imefikiwa kati ya serikali na wananchi”, alisema ofisa huyo.

Aidha alisema kupitia mpango mkakati wa serikali, wananchi wamehamasishwa kuanzisha miradi ya ufugaji wa nyuki ambapo jumla ya mizinga ya kisasa 300 imesambazwa kwa wafugaji na kupatiwa fursa ya soko la ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo, alisema katika kuendeleza sekta ya maliasili katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi huu yaani mwaka 2015-2020 CCM ilielekeza kutekelezwa mambo mbalimbali ikiwemo.

Sambamba na hilo, lakini afisa huyo alisema kuwa serikali inaendelea kusimamia uzalishaji wa asali kutoka tani 5 mwaka 2014, hadi kufikia tani 10 mwaka 2020 na kuendeleza kazi ya upatikaji na usambazaji wa miche ya misitu na kuhamasisha upandaji na utunzaji wa miti.

“Katika kipindi cha miaka 10 sekta hiyo imepiga hatua kubwa ya maendeleo ambapo ilani ya Chama cha Mapinduzi ya miaka 10 inayoelekea kumaliza muda wake imetekelezeka kwa vitendo”, alisema.

Aidha alisema Idara imetekeleza Mapitio ya Sera ya misitu ya mwaka 1995, sheria ya misitu ya mwaka 1996 na mpango wa usimamizi wa misitu 2015-2025 yanaendelea.

Anasema kanuni Na.17 ya mwaka 2013 ya usimamizi wa maliasili zisizorejesheka imekamilika.

IDARA YA MISITU

Kuhusina na sekta ya misitu, ofisa huyo alisema katika kipindi hiki cha miaka kumi ya uongozi wa Dk Ali Mohamed Shein Idara ya Misitu imefanikiwa kufanya mambo mbalimbali ya maendeleo.

Alisema Idara imefanikiwa kununua tani mbalimbali za maliasili zisizorejesheka zipatazo 1,443,442 ikiwemo mchanga tani 1,072,345, kifusi tani 87,855, kokoto tani 112,250 na mawe tani 170,990) ambazo zilichimbwa na kusafirishwa.

“Katika kipindi hicho tulifanya Doria 225 katika maeneo ya hifadhi za misitu na katika usafirishaji wa maliasili zisizorejesheka ambapo gari 143 zimekamatwa na matukio 230 yameripotiwa kwa makosa ya usafirishaji wa maliasili na uharibifu wa mazingira”, alisema.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, akipima mti kujua upana wake baada ya kuzindua zoezi la sensa ya miti (woody Biomass Survey) katika hifadhi ya Taifa ya msitu wa Jozani akiwa moja katika hafla ya uhifadhi wa misitu.

Kwa upande wa Misumeno ya moto, Afisa huyo alisema maofisa wake wamekamata misumeno 84 huku 25 ikichomwa moto Unguja na iliyosalia imehifadhiwa kwa matumizi ya dharura.

Ofisa huyo alisema hekta 99.5 zimepandwa miti ya Mikeshia, Mijohoro, Minazi na Miti ya Matunda katika maeneo matano yaliyochimbwa mchanga Mangapwani, Zingwezingwe, Donge chechele, Kidanzini na Fujoni Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.

KUIMARISHA MAENEO YA HIFADHI

Kama Ibara ya 78 (b) ya CCM imeagiza hivyo, idara imefanikiwa kuimarisha maeneo ya hifadhi na usimamizi wa wanyama pori walio hatarini kutoweka wakiwemo Paa nunga, Kima punju na Popo wa Pemba ili kuongeza idadi ya wanyama hao na kuimarisha utalii wa kimaumbile (eco-tourism).

Hata hivyo alisema Idara imefanikiwa kutekeleza kwa vitendo hasa katika hifadhi nne za Taifa ya Jozani, Masingini, Kiwengwa-Pongwe na Ngezi- Vumawimbi zimepandishwa hadhi mwaka 2017 kwa mujibu wa Sheria ya misitu ya mwaka 1996.

Ofisa huyo aliongeza kuwa maeneo miundombinu ya utalii yameimarishwa ikiwemo kituo kipya cha utalii (Zanzibar city Park- Masingini) sehemu za mapumziko, huduma za ofisi ya kituo, njia za kupitia watalii, mnara wa kuangalia haiba ya mji wa Zanzibar, ujenzi wa vyoo na mkahawa katika hifadhi ya Maumbile Masingini.

hifadhi ya jozani

Sambamba na hilo, alisema kwa kuwa makobe ni miongoni mwa mali asili wanaohifadhiwa msitu tengefu waliweza kuokolewa na serikali wakati wakitaka kusafirishwa nje ya nchi.

“Tulifanikiwa kuwaokoa makobe wapatao 250 huko Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume mwaka 2015 wakijaribu kusafirishwa nje ya nchi bila ya kuwa na vibali”, alisema.

Aidha, alisema makobe 185 kati yao walifariki kutokana na mfumo mbaya uliotumiwa kuwasafirisha pamoja na mazingira ya kuwahifadhi wanyama hao. 

Kuhusiana na uhifadhi wa wanyama pori, ofisa Miza alisema idara imefanikiwa kuyatunza mazizi 10 ya wanyamapori ambayo kwa sasa yanatambuliwa  kuwa na aina nne za wanyama ya reptilia 32, samaki sita, mamalia 38 na ndege 27).

Hata hivyo alisema tayari kwa sasa wamekamilisha kanuni za usimamizi na uhifadhi wa misitu na wanyamapori zikiwemo kanuni ya hifadhi ya Taifa ya Jozani, kanuni ya hifadhi za maumbile (Ngezi na Masingini) na kanuni ya uhifadhi wa kimataifa wa wanyama waliohatarini kutoweka (CITES).

USIMAMIZI ENDELEVU WA RASLIMALI

Ofisa huyo alisema kwa mujibu wa ibara ya 78 (c) imelenga kusimamia matumizi endelevu ya rasimali za misitu ya jamii na kuongeza kiwango cha uzalishaji wa asali kutoka tani 5 mwaka 2014, hadi kufikia tani 10 mwaka 2020.

Alisema Idara imetoa mafunzo ya ufugaji nyuki kwa wilaya za kati, Kusini na Kaskazini ‘A’ na ‘B’ ambapo walengwa 50 (35 wanawake na 15 wanaume) wameshiriki.

“Vituo viwili vya Masingini Unguja na Makuwe kwa Pemba vimeanzishwa kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wafugaji wa nyuki, huku wafugaji wengine 962 wa nyuki wakitambuliwa 524wakiwemo wanawake na 438 wanaume)”, alisema.

Sambamba na hilo, alisema jumla ya tani 5.3 za asali zimezalishwa kwa mwaka 2017 (Unguja 1.7 na Pemba 3.62 huku wanakamati 62 kutoka shehia na kamati za uhifadhi wa misitu ya jamii 31 (21 Unguja na 10 Pemba wakipatiwa mafunzo ya uhifadhi na usimamizi wa mistu ya jamii.

Pia Miza alisema mikutano miatu iliyowashirikisha wanakamati 45 (wanawake 15 na wanaume 30) wa shehia 20 zinazozunguka hifadhi ya Taifa Jozani na Jambiani – Muyuni ilifanywa kwa lengo la kuwapatia mafunzo ya usimamizi wa mikataba ya misitu.

Alisema katika kipindi hicho, jumla ya mikataba 12 ya usimamizi wa rasilimali za misitu imo katika hatua za mwisho za uwekaji wa saini kwa ajili ya kukabidhiwa wananchi kwa utekelezaji.

UKATAJI NA USAMBAZAJI WA MICHE

Kuhusiana na ukataji wan a usambazaji wa miche, Ofisa huyo alisema ibara ya 78 (d) ya CCM ililenga kuendeleza kazi ya uatikaji na usambazaji wa miche ya misitu ili kuongeza upandaji na utunzaji wa miti.

Hivyo, katika sekta hiyo Ofisa huyo alisema Idara imefanikiwa kutekeleza mambo mbalimbali ambapo jumla ya miche 3,698,922 imeoteshwa katika vitalu vya Serikali, kati ya hiyo miche ya Misitu 2,775,289 (Unguja 2,639,453 na Pemba 135,836) miche ya matunda na viungo 638,907 (Unguja 578,154 na Pemba 60,753) imesambazwa kwa ajili ya kupandwa.

Alisema hekta 263 (Chaani 97.9, Kibele 35.4, Dunga 31.1, Unguja Ukuu 47.8 na Maziwa Ng’ombe hekta 22.7) zimepandwa miti katika mashamba ya serikali na hekta 24.6 zimepandwa miti katika hifadhi za serikali (Kiwengwa, Masingini na Jozani). Aidha hekta 116.5 zimepandwa miti ya mikoko Unguja na Pemba.

Miza aliongeza kuwa miche 950,000 imeoteshwa na wanajamii ambapo hekta 383 zimepandwa miti katika maeneo yaliyo wazi ikiwemo miti ya matuda, misitu, viungo pamoja na mikarafuu.

MAZAO YA BIASHARA

Akizungumza kuhusiana na mazao ya biashara, ofisa huyo kwa mujibu wa ibara 78(e) alisema Idara ilipanga kuzalisha na kupanda mazao ya biashara na matunda ikiwemo Minazi, Mikarafuu, Manjano, Iliki, Tangawizi, Pilipili manga, kungumanga na kufanya utafiti mazao mapya ya matunda na biashara.

Hata hivyo alisema Idara imefanikiwa kutekeleza mambo mbalimbali ikiwemo kuotesha miche ya mikarafuu 975,245 (Unguja 320,776 na Pemba 654,469) katika vitalu vya Serikali na mikarafuu 484,253 (Unguja 85,571 na Pemba 398,682) katika vitalu vya watu binafsi.

Alisema miche ya matunda na viungo 590,531 (Unguja 371,307 na Pemba 219,224) imeoteshwa kupitia vitalu binafsi. Aidha, vitalu binafsi 101 vimepatiwa vifaa vya uoteshaji miche (Keni 35, Mapauro 19, Reki 19 na Vifuko kilo 87).

Wakati tunashuhudia kumalizika kwa awamu ya saba ya uongozi wa Rais Dk. Shein mengi yametekelezwa katika Idara ya misitu na mafanikio makubwa yamepatikana.