Vikosi maalumu vyajengewa uwezo

NA MARYAM HASSAN

UONGOZI wa awamu ya saba ulio chini ya Rais anaemaliza muda wake wa uongozi, Dk. Ali Mohamed Shein ni wa kupigiwa mfano kutokana na kutekeleza vyema ilani ya chama cha Mapinduzi.

Kwa mnasaba huo, utelekezaji wa Ilani umekwenda sambamba na kauli za aliyekuwa Rais wa kwanza Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.

Kauli zao na ilani ya Chama cha Mapinduzi ni kuhakikisha kuwa nchi inabaki kuwa salama na wananchi wake kushiriki kazi za kijamii kwa amani na utulivu.

Akiwa kiongozi kwa vipindi viwili Dk. Shein, yapo mengi ameyafanya kiasi cha kwamba hata yakielezwa hayawezi kumalizika.

Dk. Shein aliimarisha mambo mengi ikiwemo huduma za afya, elimu, maji safi na yaliyoachwa na maraisi waliopita.

Makala haya maalumu inazungumzia jinsi serikali ilivyoimarisha huduma za uokoaji kwa kuona umuhimu wake kwa jamii hasa pale yanapozuka maafa na majanga mbali mbali.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2010-2015) yapo mafanikio mengi yamepatikana, ikiwemo kuanzishwa kwa sera ya maafa ya mwaka 2011.

Sera hiyo imeandaliwa pamoja na kuwekwa kwa mipango ya elimu ya kukabiliana na maafa kwa wananchi umetekelezwa.

Aidha kwa kuona umuhimu wa kuanzishwa kwa Kamati ya Maafa ya Zanzibar, wilaya na shehia 277 zimeendelea kuimarishwa na kupatiwa mafunzo ya msingi ya kukabiliana na maafa.

Sambamba na hayo, serikali imeimarisha kikosi maalum cha uzamiaji ili kuona kwamba zinafanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa.

Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa mwaka 2015-2020 imesema itahakikisha inasimamia utekelezaji wa sheria ya kukabiliana na maafa pamoja na kuanzisha Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa.

Mkurugenzi Mtendaji Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, Makame Khatib Makame, akizungumza na makala haya alisema utekelezaji wa ilani ya chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020, chini ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekifanya kikosi hicho kuwa cha kipekee hasa kwa kukipa nyenzo bora za uokozi.

Alisema miongoni mwa hayo ni kuanzishwa kwa sheria nambari 1 ya mwaka 2015 ambayo iliipa mamlaka ya kuazishwa Kamisheni ya kukabiliana na maafa Zanzibar, ikiongozwa na Mwenyekiti wake ni Makamo wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, na wajumbe wake ni mawaziri wote wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kushirikiana na wakuu wa Vikosi vya SMZ, na wakuu wa mikoa wote, pamoja na Mkurugenzi wa Shirika la Bandari.

Alifahamisha kwa mujibu wa sheria hiyo pia kumeanzishwa kwa kamati ya kitaalamu ya kukabiliana na maafa, ambayo ipo chini ya Mwenyekiti Katibu Mkuu Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais na wajumbe wake ni makatibu wakuu wote wa SMZ.

Vile vile alieleza kuwa maafisa tawala wa vikosi ni wajumbe wa kamati ya kitaalam wakiwemo na makatibu tawala wa wilaya.

“Kwa msingi huo unaonesha kuwa kuanzishwa kwa sheria hiyo kunaonesha wazi kuwa jinsi gani wanaweza kukabiliana na maafa pindi yanapotokea kuanzia ngazi ya shehia”, alisema.

Alivitaja vituo vinavyotoa huduma kuwa ni pamoja na Gamba, Maruhubi, Makunduchi kwa Unguja na Pemba ni Micheweni, Chake Chake na Mkoani.

Kuhusu suala la elimu, Makame alisema wameweza kuzifikia ngazi zote za wilaya na shehia huku wavuvi nao waliweza kupatiwa elimu.

Sambamba na hayo alieleza kuwa elimu ya maafa ilifikiwa katika skuli mbali mbali za Unguja na Pemba pamoja na vyama vya siasa huku makundi maalum yaliweza kupatiwa elimu ya kujikinga na maafa.

Aidha kamisheni ya kukabiliana na maafa Zanzibar imeweza kujengea nyumba familia 30 kwa upande wa Unguja katika maeneo ya Nungwi na Pemba nyumba 30 maeneo ya Tumbe.

Mkurugenzi huyo alitanabahisha kwamba mradi wa ZUSP umeweza kuleta mafanikio makubwa hasa katika mkoa wa Mjini Magharibi kwa kuweza kujenga mitaro ya kisasa ambayo imeweza kuwakomboa wananchi wa mkoa huo kwa sababu walikuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya nyumba zao kujaa maji na wengine kupoteza maisha.

“Mradi huu umeweza kuwa mkombozi kwa wakaazi wa maeneo mbali mbali ya mji wa Zanzibar ambao uliosimamiwa na Meneja wa mradi wa huduma za jamii”, alisema.

Aidha Mkurugenzi huyo wa maafa Ali alisema tatizo la kutuama kwa Maji ya Mvua katika maeneo ya Mji wa Zanzibar linatarajiwa kuondoka hivi karibuni pale ambapo Mtaro Mkuu unaotokea Bwawa la Mwanakwerekwe, kupita Bwawa la kwa Mtumwa Jeni, kuelekea Bwawa la Sebleni litakapounganishwa na mtaro wa Mikunguni na maji hayo kumalizikia Bahari ya Kinazini.

Pamoja na hayo mfuko wa maafa katika kipindi hicho cha uongozi wa Dk. Shein umejenga maghala matatu ya kuhifadhia vifaa kati ya hayo Unguja ni mawili na moja Pemba.

Alivitaja baadhi ya vifaa hivyo ni pamoja na mahema life jacket, mobile toilet, vitanda, magodoro, mablanket na vifaa vyenginevyo.

Sambamba na hayo, lakini Mkurugenzi huyo alisema serikali imeanzisha mpango wa kutokomeza kipindupindu ambapo mpango huo ni wa miaka 10.

“Mpango huo umeanza kutekelezwa tokea mwaka 2018 na unatarajiwa kumalizika mwaka 2027 kama ilivyotokomezwa malaria Zanzibar”, alisema.

KIKOSI MAALUM CHA KUZUWIA MAGENDO (KMKM)

Kwa mujibu wa taarifa za Luteni Haji Mussa Haji kutoka kuzuia magendo (KMKM) ameeleza kuwa, uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein umeibua miradi mingi ambapo kabla ya hapo haikuwepo.

“Kamisheni ya kukabiliana na maafa imeweza kushirikiana vyema na vikosi vya ulinzi na usalama ikiwemo KMKM ambapo imeimarisha ujenzi wa vituo vya uokozi ikiwemo Nungwi, mkoani Pemba, Kibweni na vyote hivyo vimewezeshwa kwa kupatiwa vifaa vya uokozi, alisema Luteni Haji.

Aidha alisema vituo hivyo vimefungwa vifaa maalum vya mawasiliano na kuweza kuwa na mifumo mitatu ijulikanayo kwa majina ya VMS, Sea Vision na Find Ship.

“Mifumo hii imekuwa na faida nyingi zikiwemo upatikanaji wa taarifa kwa urahisi kutoka kwenye vyombo vya baharini na wananchi na kuimarisha mashirikiano baina ya KMKM na ZMA, MRCC pamoja na vyombo vya ulinzi vya Jamhuri ya Muungano Tanzania hususan Jeshi la Wananchi Tanzania na Uhamiaji.

“Hivyo uwepo wa vituo vya uokozi kunahakikisha upatikanaji wa huduma za uokozi, uzamiaji na ulinzi wa nchi na kuepusha majanga ya uzamaji wa vyombo vya baharini na athari za maisha ya wananchi.

Alieleza kuwa mpaka sasa kikosi hicho kimekuwa na mabadiliko makubwa ikiwemo kuweza kudhibiti magendo sambamba na suala zima la maafa ya baharini.

Luteni Haji aliongeza kuwa uongozi wa Dk. Shein umewapatia boti saba zenye mwendo kasi zikiwa zimegharimu kiasi cha shilingi bilioni 15.5, zenye uwezo wa kuchukua watu 400 hadi 600 kwa wakati mmoja pindi yanapotokea maafa.

Sambamba na hilo, alisema ndani ya uongozi wake imejengwa hospitali kubwa na ya kisasa kwa ajili ya kutoa huduma zote ambayo nayo iligharibu bilioni 2.8 pamoja na vifaa tiba pamoja na ujenzi wa kambi saba huku nyengine zikifanyiwa matengenezo.

KIKOSI CHA ZIMAMOTO NA UOKOZI (KZU)

Kikosi cha Zimamoto na Uokozi kimeanzishwa chini ya  Sheria namba 7 ya mwaka 1999 iliyopitishwa na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Kikosi hicho nacho hakiko nyuma katika kutoa ushirikiano pindi yanapotokea majanga, ambapo uongozi wa Dk. Shein umekiona kikosi hicho kwa kukipatia vifaa mbali mbali.

Hongera Dk. Shein kwa kutekeleza vyema ilani ya Chama cha Mapinduzi, wananchi wote wa Zanzibar wanakutakia mapumziko mema baada ya kumaliza kuwatumikia bila ya kuwakwaza.