NA ABDI SULEIMAN

ASASI za kiraia zimeshauriwa kuiga mfano wa taasisi ya Milele Zanzibar Foundation, kuisaidia serekali katika nyanja mbali mbali za kijamii ikiwemo sekta ya elimu.

Ushauri huo umetolewa na Msaidizi Mkurugenzi elimu ya maandalizi na msingi, kutoka Halmashauri ya wilaya ya Micheweni, Tarehe Khamis Hemed, katika hafla ya kuadhimisha siku ya kujua kusoma na kuandika duniani, iliondaliwa na taasisi ya Milele Zanzibar Foundation.

Alisema sekta ya elimu inakumbana na changamoto mbali mbali kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya matumizi ya vitabu kwa wanafunzi.

“Sekta ya elimu imekua sana, kila mwaka watoto wengi wanaandishwa skuli kwa kiasi kikubwa wananchi hasa huku Micheweni wameelimika jambo hili ni faraja kwetu, lakini kuna changamoto kubwa ya vitendea kazi,” alisema.

Alisema Milele iko mstari wa mbele kusaidia elimu na huduma nyengine za kijamii na kuziomba taasisi nyengine kuiga mfano huo.

Aidha aliwataka wanafunzi kuendelea kusoma kwa bidii, ili kuwa wataalamu wazuri wa hapo baadae ili kusaidia jamii ya Micheweni.

Mwakilishi Milele Zanzibar Foundation, Aisha Juma Mussa, alisema taasisi hiyo itaendele kuunga mkono juhudi za serekali ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora.