NA HUSNA MOHAMED

MNAMO mwezi wa Novemba mwaka huu wanafunzi wa kidato cha nne nchini wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya mwisho ya kumaliza elimu ya lazima.

Katika kujiandaa na mitihani hiyo wanafunzi hao bado hawajachelewa na kwamba wanatakiwa kusoma kwa bidii ili kuona wanafaulu mitihani hiyo ili kuendelea na masomo ya sekondari ya juu.

Pamoja na maandalizi hayo lakini bado wanafunzi hao wasisahau tahadhari juu ya ugonjwa wa corona na namna ya kujikinga na kutokomeza maradhi hayo.

Huku mitihani hiyo ikikaribia, lakini pia taifa la Tanzania linakabiliwa na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi ujao, hivyo uchaguzi huo usichukuliwe kuwa kigezo cha kutofanya vyema mitihani hiyo.

Kwa mujibu wa wizara ya elimu na mafunzo ya amali Zanzibar kupitia Idara ya elimu ya Sekondari inawasisitiza wazazi, walimu na wananchi wote kuendelea kuwasimamia watoto na wanafunzi wote kwa ujumla kwa masuala ya kiafya na ya kielimu.

Hivyo basi wizara hiyo imewataka wazazi, walezi na wananchi wote kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi kuwasisitiza wanafunzi kututoshiriki na kufuata makundi bali kujikita katika masomo yao.

Sambamba na hilo lakini pia jamii inasisitizwa kuchukua nafasi yao na kuhakikisha muda mwingi watoto wanakuweko nyumbani na kudurusu masomo yao ipasavyo.

Pia ili kuona wanafunzi wanakamilisha  mitaala yao ipo haja kwa walimu kuhakikisha kuwa wanatoa kazi za kutosha ikiwa ni moja ya maandalizi ya mitihani yao.

Ili kuona hayo yote yanafanikiwa ni lazima wanafunzi kujitambua na kujua wao ni walengwa zaidi wa wengine hivyo kusoma kwa bidii ni njia ya kuwafikisha kule kulikokusudiwa.

Bila ya shaka serikali kupitia wizara yake ya elimu iko katika kukamilisha maandalizi ya mitihani hiyo, huku tukiamini pia wanafunzi wanaendelea kujiandaa kama tulivyoeleza hapo awali.

Wakati wa mitihani itakapowadia tunawanasihi wanafunzi wote kuhakikisha kuwa wanakuwa watulivu katika mitihani na kuifanya kwa uelewa mkubwa.

Udanganyifu katika mitihani kwa kipindi cha maandalizi na wakati wa mitihani  hauna nafasi kwani kufanya hivyo kutawaezesha wanafunzi hao kukamatwa ama kutofanya vyema.

Sambamba na hilo lakini tunawaomba pia wanafunzi kukataa kabisa kudanganywa kwa kupewa ‘paper’ za uongo ambazo zitawapotezea kabisa malengo yao ya matayarisho ya masomo kwa ajili ya mitihani.

Wanafunzi iwapo watakuwa wamejitayarisha vyema kwenye mitihani hio, basi tunaamini kuwa hawatakubali kudanyanywa kwa hali yoyote.

Iwapo wanafunzi hao watafuata nasaha hizi na kufanya mitihani yao vyema, basi watakuwa ni viongozi na wataalamu wa miaka ya mbele wa kada tofauti.

Tunawatakia kila la kheri wanafunzi wetu wa kidato cha nne katika mitihani yao na tunawaomba kufanya vyema kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.