NI miaka 30 imetimia tangu Umoja wa Mataifa ulipopitisha azimio la haki za mtoto, ambapo katika kipindi hicho cha miongo mitatu kumepatikana mafanikio makubwa katika utekelezwaji wa azimio hilo.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa hivi karibuni imeelezea utafiti uliofanywa na shirika la Umoja huo la UNICEF umeeleza kuwa nchi nyingi zimejitahidi kutekeleza azimio hilo.
Aidha ripoti hiyo pia imesisitiza na kutoa wito kwa mataifa kuhakikisha yanatekeleza wajibu wao kikamilifu katika utekelezwaji wa azimio hilo.
Katika taarifa yake aliyoitoa siku ya kuadhimisha miaka 30 tangu kuasisiwa kwa azimio hilo, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, aliyataka mataifa duniani kuhakikisha yanawajibika katika kuwapatia haki watoto.
Katibu huyo alibainisha kuwa tangu wakati huo kumefikiwa hatua kadhaa na kueleza kuwa kuna umuhimu wa kuunganishwa nguvu zaidi na kuhakikisha kila mmoja anawajibika ipasavyo katika utekelezwaji wa makubaliano hayo hasa ikizingatiwa kuwa bado watoto wanakabiliwa na vitisho.
Guterres alisema nchi zote zilitambua hali ya hatari ya kipekee inayokabili watoto na kuahidi kuwapatia chakula, huduma ya afya, elimu na ulinzi na kwamba tangu wakati huo, kumekuwepo na maendeleo.
Mathalani alisema idadi ya vifo vya watoto imepungua kwa zaidi ya nusu na udumavu wa watoto ulimwenguni umepungua ingawa bado mamilioni ya watoto bado wanakabiliwa na vita, umaskini, ubaguzi na magonjwa.
Hata hivyo alisema, “ulimwenguni kote, watoto wanatuonyesha uthabiti na uongozi wao wakichechemua ulimwengu endelevu zaidi kwa wote. Tunapoadhimisha miaka 30 ya mkataba huu muhimu, nasihi nchi zote zitime ahadi zao. Tusongeshe maendeleo tuliyofikia na tuahidi kujali watoto kwanza. Kila haki kwa kila mtoto.”
Guterres alisema ikiwa imefikia miaka 30 tangu kupitishwa kwa azimio hilo muhimu, aliwasihi viongozi wote duniani kuhakikisha wanatimiza ahadi zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi mkuu wa UNICEF, Henrietta Fore alinukuliwa akisema ingawa kuna ongezeko la idadi ya watoto wanaoishi maisha bora na wakiwa na afya njema, lakini kundi jingine linaloishi katika hali ya umasikini bado linakabiliwa na kitisho kikubwa.
Mkurugenzi huyo alisema katika miongo mitatu baada ya azimio hilo, kumeonekana mafanikio makubwa katika kupunguza idadi ya watoto wanaoshindwa kujiunga na skuli za msingi kwa karibu asilimia 40, huku idadi ya watoto wa chini ya miaka mitano wanaodumaa ikipungua kwa zaidi ya milioni 100.
Henrietta Fore alisema hata ugonjwa wa polio uliokuwa ukisababisha takriban watoto 1,000 kupooza kila siku katika miongo mitatu iliyopita, hivi sasa asilimia 99 ya visa hivyo vimeondolewa.

Pamoja na hayo mkurugenzi huyo alionya hatari ya mabadiliko ya tabianchi ambayo inatishia mafanikio yaliyopatikana hasa kwenye suala la lishe, elimu na afya.
Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa tishio jengine kubwa dhidi ya haki za watoto liliopo duniani hivi sasa ni unyanyasaji wanaofanyiwa kupitia kupitia mitandao ya kijamii.
Aidha, alisema umasikini, kukosekana kwa usawa na ubaguzi pia vimeendelea kuwanyima mamilioni ya watoto haki zao kila mwaka huku watoto 15,000 walio chini ya miaka mitano wakiwa wanafariki dunia kila siku.
Idadi hiyo ya watoto wanaopoteza maisha inatokana na magonjwa yanayoweza kutibika na vyanzo vya maradhi hayo vinaweza kuzuilika kama vile uzito uliopitiliza kwa watoto na wasichana wanaopata tatizo la upungufu wa damu.
Siku ya mtoto duniani ilianzishwa mwaka 1954 kufuatia Azimio la Ulimwengu la siku ya mtoto na hudhimishwa kila Novemba 20 ya mwaka kuhamasisha ustawi wa watoto duniani.
Siku ya mtoto duniani ilianzishwa mwaka 1954 na huadhimishwa tarehe 20 mwezi Novemba ya kila mwaka ili kusongesha utangamano na ustawi wa kimataifa miongoni mwa watoto wote duniani.
Tarehe hii ni muhimu kwa kuwa ndio ambayo mwaka 1959 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio la Haki za Mtoto na pia ni tarehe ambayo mwaka 1989 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto, CRC.
Tangu mwaka 1990, siku ya kimataifa ya mtoto imekuwa ikiadhimishwa kutambua tarehe hiyo 20 ya mwezi Novemba ambapo Baraza Kuu lilipitisha azimio kuhusu haki za mtoto na pia Mkataba wa kimataifa kuhusu haki za mtoto.
Ni vyema kutambua kuwa akina mama, baba, walimu, madaktari, viongozi wa serikali, wanaharakati, viongozi wa dini, viongozi wa kampuni, wanahabari nguli pamoja na vijana na watoto wenyewe wanaweza kuwa na dhima muhimu katika kuifanya siku hii ya kimataifa ya mtoto iwe muhimu zaidi kwenye jamii na nchi zao.
Siku hii pia ni hamasa pia katika kuchechemua na kufurahia haki za mtoto, na kuziweka kivitendo na hivyo kufanya dunia iwe bora zaidi kwa watoto.
Zaidi ya watoto milioni saba kote duniani wanakabiliwa na aina mbalimbali za mateso katika vituo mbalimbali maalumu ikiwemo vituo vya mahabusu vya uhamiaji, vituo vya polisi, magereza na maeneo mengine ya mahabusu.
Hayo ni kwa mujibu wa matokeo ya utafiti yaliyotolewa na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, (OHCHR) mjini Geneva, Uswisi ikiongeza kuwa ni bayana kwamba hali hiyo inakwenda kinyume na matakwa ya mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto (CRC).
“Uwekaji mahabusu watoto uwe tu kama suluhu ya mwisho kwa kwa kipindi kifupi cha muda wa unaostahili. Hii inamaanisha kwamba watoto kimsingi hawastahili kuwekwa rumande na serikali zinapaswa kila wakati kutafuta mbinu mbadala badala ya kuwasweka rumande au kuwatupa magereza watoto.”