NA TATU MAKAME

MKURUGENZI Kampeni Jimbo la Mahonda, Mwinyi Jamali Ramadhani, amewataka wanachama wa CCM Jimbo la Mahonda kuwachagua wagombea wa chama hicho, ili walete maendeleo katika kipindi kijacho.

Jamali alisema hayo wakati akizungumza na WanaCCM katika Uwanja wa Mpira Kiwengwa kumbaurembo ikiwa ni muendelezo wa kuwaombea kura wagombea wa nafasi mbalimbali ikiwemo Urais, Ubunge, Uwakilishi na Udiwani kwa viongozi wanaomba ridhaa ya kuomba kura ili waongoze Jimbo hilo.

Mkurugenzi huyo ambae pia ni Meneja Kampeni Jimbo hilo, alisema chama cha Mapinduzi ndicho chenye uwezo wa kuleta mabadiliko hivyo aliwataka wanachama kuwapa kura viongozi hao ifikapo Oktoba 28 mwaka huu.

Alieleza kuwa viongozi waliomo madarakani akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, alitekeleza mambo mengi ya maendeleo ikiwemo huduma za jamii hivyo aliwataka wananchi kuwachagua wagombea, ili kushirikiana na Rais atakaeingia madarakani kuendeleza huduma za jamii.

“Chama cha Mapinduzi ndicho chenye misingi mizito na kufanya kazi kwa miongozo ya sheria na kanuni hivyo wachaguweni wagombea wa CCM waendeleze kuleta maendeleo katika nchi yetu”, alisema Jamali.