NA ABOUD MAHMOUD

WAFANYAKAZI wa Shirika la Bandari Zanzibar wametakiwa kuwa wazalendo, waadilifu na wenye nidhamu katika kuleta maendeleo ya kazi zao kila siku.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Abdullah Juma Abdullah wakati alipokua akizungumza na wafanyakazi kwenye kikao cha kuagana nao akiwa amemaliza muda wake wa kutumia utumishi wa Serikalini katika ukumbi wa bandari Malindi mjini Unguja.

Mkurugenzi huyo mstaafu alisema bila ya kuwa mambo hayo matatu maendeleo na mafanikio kwa shirika na wao binafsi hayawezi kupatikana .

“Napenda kutoa ushauri wangu kwenu, ili muweze kufanikiwa nyinyi wenyewe pamoja na shirika kwa ujumla ni vyema kuwa wazalendo na naamini mkikubaliana na hilo na kuwa waadilifu naamini mtafika mbali kimaendeleo kwenu na shirika kwa ujumla,”alisema.

Mstaafu huyo, alisema hata kama mtumishi ana elimu ya kiwango cha juu, lakini bila ya kuwa na nidhamu katika kazi yake hawezi kufika popote na hatopata mafanikio.

Alisema ni vyema watumishi wa Shirika hilo kuachana na tabia kutiliana fitina na kupikiana majungu kwa maslahi ya mtu mmoja, jambo ambalo linazorotesha ufanisi wa taasisi.

“Tumekua na tabia ya kupikiana majungu na kutiliana fitna hilo sio jambo zuri nakuombeni tuachane na hili jambo, ili tuweze kufika mbali, kama tutaendekeza mambo hayo hamtokua na ufanisi mzuri,”alifafanua.