PARIS,UFARANSA

TUME ya Ulaya imependekeza kuwa Umoja wa Ulaya,EU uwekewe lengo la kupunguza utoaji wa gesi chafuzi kwa mazingira kwa asilimia isiyopungua 55 kufikia mwaka 2030 kutoka viwango vya mwaka 1990.

Hiyo kwa kiasi fulani inaelezea nia kuu zaidi kuliko lengo la sasa la upunguzaji gesi hizo kwa asilimia 40.

Rais wa tume hiyo Ursula von der Leyen aliwasilisha pendekezo hilo kwenye Bunge la Ulaya katika hotuba yake ya kwanza ya nchi wanachama wa umoja huo tangu ashike madaraka mwaka jana.

Kabla ya kuwasilisha lengo hilo, von der Leyen alisema,ingawa sehemu kubwa ya shughuli za kiuchumi duniani zilisimama wakati wa marufuku ya kutotoka nje na chumi kufungwa, dunia inaendelea kuwa na joto la kiwango hatari.

Tume hiyo inaitaka EU kuchukua jukumu katika kupambana na ongezeko la joto duniani kwani Marekani inasema inajiondoa katika Makubaliano ya Paris ya mabadiliko ya tabia nchi.

Lakini bado haijulikani iwapo nchi zote wanachama wa EU zitaunga mkono lengo hilo kwani baadhi ya nchi hizo bado zinategemea nishati inayozalishwa kwa makaa ya mawe inayochangia kiwango kikubwa cha gesi chafuzi kwa mazingira.