TRIPOLI,LIBYA

MKUU wa Serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa Fayez Serraj amesema ananuia kukabidhi madaraka kwa mtu mwengine ifikapo mwishoni mwa mwezi Oktoba,wakati mazungumzo yakiendelea kutafuta suluhisho la mzozo nchini mwake.

Akizungumza kwa njia ya televisheni usiku wa kuamkia jana, Serraj alisema majadiliano kati ya pande hasimu nchini Libya yaliifikisha nchi hiyo katika kipindi kipya cha maandalizi ya kuziunganisha taasisi za kitaifa na kutayarisha uchaguzi wa bunge na wa rais.

Mapema mwezi huu,pande hizo ziliafiki uchaguzi katika muda wa miezi 18 na kuiteuwa Serikali mpya,na zinatarajiwa kukutana tena siku za hivi karibuni kwa mazungumzo zaidi.

Serraj alichaguliwa mwaka 2015 kuliongoza baraza la kitaifa, lililoundwa na makundi mbali mbali ya kisiasa katika mkutano uliofanyika mjini Skhirat, Morocco.