TAYARI wawakilishi wa Zanzibar kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao wamepatikana baada ya kukamilika kwa msimu wa 2019/2020.
Wawakilishi hao ni Mlandege ambao watatuwakilisha kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na maafande wa Kikosi cha Valantia (KVZ), watakaocheza Kombe la Shirikisho.

Wakati Mlandege ndiyo mabingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar, KVZ tiketi yao imepitia michuano ya Kombe la FA wakiwa ndiyo mabingwa.
Tunachukua nafasi hii kuwapongeza wawakilishi wetu baada ya kufaulu mitihani mliyopitia na hivyo sasa kupewa jukumu la kupeperusha bendera ya Zanzibar kwenye michuano hiyo mikubwa ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).

Ni imani yetu kuwa hamtatuangusha baada ya kujidhihirisha kwamba mlistahili kuitwa mabingwa kutokana na jitihada na viwango mlivyovionesha kwenye ushiriki wenu.

Baada ya kukata tiketi hizo, Zanzibar Leo kama mdau wa michezo tungelipenda kuzishauri Mlandege na KVz sasa kuanza maandalizi ya mapema, kwani siku zimeisha ni takriban siku 80 zimebakia kabla ya kuanza kwa michuano hiyo.
Hivyo huu ni wakati muafaka wa kuanza maandalizi kwa timu hizo kwa lengo la kuhakikisha zinafanya vizuri na kuendelea kuwatoa kimasomaso Wazanzibari katika michuano ya kimataifa, hasa ikizingatiwa kwa miaka kadhaa hatujakuwa na ushiriki mzuri katika mashindano hayo.

Lakini ni vyema maandalizi hayo yakaenda sambamba na kutafuta mechi nyingi za kujipima nguvu ikiwemo kucheza na timu hata kutoka nje ya visiwa hivi katika kuangalia ubora wa wachezaji kwenye michezo hiyo.
Ili tusionekane kama vile tumekurupuka kwenye ushiriki wetu, maandalizi ni jambo la msingi na muhimu kama tunataka kupata matokeo na mafanikio kwenye michuano hiyo.

Mipango ya maandalizi ianze kwa kuhakikisha timu zinajengewa mazingira bora na kuandaliwa programu maalum kuelekea kwenye michuano hiyo.

Tunasema hivyo kwa sababu tunajua michuano ya kimataifa si lelemama, inahitaji maandalizi mazuri na ya muda mrefu, kwa maantiki hiyo itakuwa jambo jema kwa vyombo vinavyohusika kuzisaidia timu hizo kwenye maandalizi ili zituwakilishe vyema.

Na katika hilo, sio kwa kuliachia Shirikisho la Soka la Zanzibar ( ZFF), pekee, itakuwa vyema kwa taasisi mbalimbali nazo kuchangia maandalizi hayo kwa njia moja au nyengine, kwa vile timu hizo zitakuwa zikituwakilisha taifa la Wazanzibari.

Ipo haja kama taifa kuunganisha nguvu katika kuhakikisha timu zetu zinafanya vyema na kuiletea nchi sifa kwa vile michuano hiyo ni muhimu kama taifa kuweka malengo yatakayosaidia katika mipango ya baadae ya kuendeleza na kuinua soka na michezo kwa ujumla visiwani hapa. Zanzibar yenye mafanikio ya kimichezo inawezekana ikiwa kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake.