NA MWAJUMA JUMA
JUMLA ya watoto 75 kati ya 150 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa macho utakaohusisha matatizo ya presha ya macho, uvimbe na maradhi mengineyo.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Kitengo cha Maradhi ya Macho Zanzibar Dk. Slim Mohammed Mgeni, alipozungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Mnazimmoja.
Alisema kuwa upasuaji huo utafanyika kati ya Septemba 28 hadi Oktoba 3 mwaka huu, utahusisha watoto wote wa Unguja na Pemba utafanyika katika hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja.
Alifahamisha kuwa upasuaji huo unafanyika kupitia mfuko wa serikali kwa kushirikiana na madaktari bingwa Muhimbili na ndani ya nchi.
Awali alisema kuwa upasuaji huo ulikuwa ufanyike Febuari mwaka huu lakini kutokana na kuibuka kwa janga la maradhi ya korona ilishindikana na kuamuliwa kufanyika mwezi Septemba.
Mratibu wa Huduma za Macho Zanzibar, Dk. Rajab Mohammed Hilal, alisema kuwa ukubwa wa tatizo la macho Zanzibar ni wastani wa asilimia moja ikiwa ni sawa na watu karibu 10,000 wenye matatizo ya macho Zanzibar kwa aina tofauti.
Alieleza kuwa tatizo la macho Zanzibar halipo kwa watoto bali hata kwa watu wazima hivyo aliwaomba wananchi wanapohisi kuumwa na macho kwenda katika vituo vya afya ili kupatiwa matibabu mapema na kuepusha athari zinazosabishia upofu.