JOHANNESBURG, Afrika Kusini
KOCHA, Pitso ‘Jingles’ Mosimane amejiuzulu kuwanoa mabingwa wa Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns ‘Masandawana’, kwa mujibu wa vyanzo vya habari nchini humo.
Imeelezwa kuwa Mosimane ameachia ngazi saa chache baada ya kupokea ofa kutoka kwa miamba wa soka Afrika na Misri, Al Ahly.

Klabu hiyo yenye historia kubwa Afrika, ipo tayari kumpa mkataba kocha huyo, baada ya kuachana na aliyekuwa kocha wao mkuu, Rene Weiler.

Mosimane anaondoka Mamelodi Sundowns huku akiacha historia ya kukiongoza kikosi cha klabu hiyo tangu mwaka 2012, akitwaa ubingwa wa Afrika Kusini mara tano, msimu wa 2013-14, 2015-16, 2017-18, 2018-19 na 2019-20.
Mbali na mataji ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini, kocha huyo ambaye aliwahi kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Afrika Kusini kuanzia mwaka 2006–2010, ameipa mataji mengine Mamelodi Sundowns kama Nedbank Cup msimu wa 2014-15 na 2019-20, Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2016 pamoja na CAF Super Cup mwaka 2017.(Goal).