MINSK, BELARUS

WALINZI wa mpaka wa Poland wamesema mpaka kati ya Belarus na Poland umesalia kuwa wazi pamoja na kwamba Rais wa Belarus Alexander Lukashenko kusema nchi yake inahitaji kufunga mipaka yake na Poland na Lithuania.

Ofisa mmoja wa Poland ambaye amekataa kutambuliwa kwa sababu hana ruhusa ya kuzungumza na waandishi habari alisema mpaka huo uko wazi na hakuna ishara kuwa utafungwa.

Lukashenko ambaye anakabiliwa na shinikizo la kujiuzulu baada ya wiki kadhaa za maandamano, alisema hapo juzi kuwa Belarus inahitaji kufunga mpaka wake na Poland na Lithuania na kuimarisha doria katika mpaka wake na Ukraine.

Belarus imetumbukia katika mzozo wa kisiasa kufuatia uchaguzi mkuu wa Agosti 9 uliogubikwa na madai ya wizi wa kura na kusababisha maandamano makubwa dhidi ya Lukashenko ambaye amekuwa madarakani tangu 1994.

Lukashenko anasema alishinda uchaguzi huo kwa njia ya haki na kuwa yeye ni mhanga wa kampeni chafu inayoendeshwa na mataifa ya Magharibi.

Rais huyo anakabiliwa na ukosoaji kutoka kwa Marekani na Umoja wa Ulaya, wakimtaka aondoke madarakani kutokana kupata ushindi wenye utata kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni.

Lukashenko alisema anawaondoa wanajeshi mitaani na kuwapeleka mipakani ili kuimarisha ulinzi hasa katika mpaka na Ukraine, huku akieleza kuwa hataki nchi yake iingie vitani.

“Sitaki nchi yangu kuwa vitani, isitoshe sitaki Belarus na Poland na Lithuania kugeuka kuwa maonyesho ya kijeshi ambako masuala yetu hayatatuliwa”, alisema rais huyo.

Aidha alifahamisha kuwa wananchi wa mataifa ya Lithuania, Poland na Ukraine kuwaeleza viongozi wa nchi hizo kwamba si vuziri kuingilia mambo ya ndani ya Belarus.