MINSK,BELARUS
MAOFISA nchini Belarus wamejaribu kumuondoa nchini humo kwa nguvu kiongozi wa upinzani Maria Kolesnikova lakini alichana hati yake ya kusafiria akipinga hatua hiyo na kuruka kutoka katika gari ili kubakia nchini humo.
Kolesnikova,mmoja wa viongozi wa mwisho ambao bado wako nchini humo wakiongoza maandamano dhidi ya rais Alexander Lukashenko, alikamatwa mpakani baada ya kutoonekana siku ya Jumatatu.
Maofisa wa mpakani walisema alikuwa anajaribu kutoroka nchini humo lakini wenzake wawili aliokuwa nao ambao waliingia nchini Ukraine walisema aligoma kufukuzwa nchini humo.
Katika mkutano na waandishi habari katika mji mkuu wa Ukraine Kiev, katibu wa habari wa baraza la uratibu la upinzani, Anton Rodnenkov , pamoja na katibu wake mkuu Ivan Kravtsov walielezea kuhusu matukio kadhaa wakati watu hao watatu wakipelekwa mpakani.