BEIJING, CHINA

MAMLAKA za China zimezidisha msako wake kwenye eneo linalojitawala la Inner Mongolia dhidi ya watu wa kabila la Mongolia wanaofanya maandamano kulalamikia hatua za kupunguza utoaji elimu katika lugha yao ya asili.

Serikali kuu ya China iliamua kuwa masomo ya lugha kwa darasa la kwanza na la saba yanapaswa kufundisha Kichina badala ya Kimongolia kuanzia muhula mpya wa masomo ulioanza mwezi huu.

Pia iliamuliwa kuwa masomo mengine yataanza kufundishwa kwa lugha ya Kichina kwa awamu kuanzia mwakani.

Wamongolia wana wasiwasi kuwa lugha yao inaweza kupotea,wakaazi wa eneo hilo walisema waandamanaji na wazazi wa watoto waliosusia masomo walikamatwa.

Mwalimu mmoja wa zamani aliiambia NHK kwa njia ya simu kuwa watu wengi walikamatwa kwa madai ya kufanya maandamano kinyume cha sheria na kuchukuliwa kama wafungwa wa kisiasa.

Shirika linalojulikana kama Southern Mongolia Human Rights Information Center lenye makaazi yake nchini Marekani linakadiria kuwa zaidi ya Wamongolia 4,000 walikuwa chini ya aina fulani ya kuzuiliwa na polisi tangu mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.