BERLIN,UJERUMANI

CHAMA cha siasa kali za mrengo wa kulia Ujerumani, AfD, kimemfukuza msemaji wake wa zamani, Christian Lüth, kwa tuhuma za kutoa matamshi yasiyo ya kibinaadamu dhidi ya wahamiaji.

Mapema, gazeti la Die Zeit lilikuwa limeripoti kwamba Lüth alizungumzia juu ya kuwapiga risasi na kuwamwagia gesi ya sumu wahamiaji mnamo mwezi Februari,wakati alipokutana na mmoja wa wanawake mashuhuri kwenye mitandao ya kijamii, Lisa Licentia, katika baa moja mjini Berlin.

Matamshi hayo yalirushwa kwenye filamu fupi iliyooneshwa na kituo kikubwa cha televisheni nchini Ujerumani, ProSieben.

Mwenyekiti mwenza wa kundi la wabunge wa chama hicho, Alexander Gauland,alisema matamshi hayo hayakubaliki na hayaendani na dhamira na sera za AfD.

Lüth anatuhumiwa kwamba wakati akizungumza na Lisa, alidai kuwa chama chake kinatumia mbinu za uchokozi ili kuvutia wafuasi, akisema kwamba kila mambo yakiharibika nchini Ujerumani, ndivyo inavyokuwa vizuri kwa AfD.