ZASPOTI
MSHAMBULIJI wa timu ya Shangani, Omar Abuu Idd, amewataka vijana wenzake kuitumia michezo kwa ajili ya kutangaza vipaji vyao kama njia ya kujipatia ajira itakayowasaidia kuendeleza maisha yao ya kila siku.


Shangani ni miongoni mwa timu inayoshiriki ligi daraja la pili wilaya ya Mjini ambapo msimu huu ilisimama katika hatua ya nne bora.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, alisema, michezo ni njia mojawapo ya kupata ajira, hivyo ni vyema kuitumia fursa hiyo kuvitangaza vipaji vyao na kuonekena.


“Endapo utaonekana na kupata nafasi ya kwenda timu kubwa utakuwa umefungua njia ya kuelekea kwenye mafanikio kama ilivyo kwa akina Feisal Salum ‘Fei Toto”, alisema.


Alisema kuna vijana wengi waliopata ajira kupitia michezo mbali mbali ikiwemo mpira wa miguu na mengine na kwa sasa wanakula maisha na familia zao kupitia tasnia hiyo na sio nyengine.


“Wapo akina Ninja, Fei, Abui na wengine wengi wapo Tanzania Bara na kuna wengine wapo katika timu za vikosi wameajiriwa”, alisema.
Hivyo, aliwataka wachezaji vijana kujiamini na kukubali kupambana kwa kila hali kwa lengo la kupata mafanikio.