NA HAJI NASSOR, PEMBA

MSHTAKIWA Khamis Othman Khamis wa Ndagoni, anayedaiwa kuhusishwa na ubakaji wa mtoto aliyechini ya umri wa miaka 18, ameiambia mahakama ya Mkoa Chake Chake kuwa, aliyembaka ana umri wa miaka 20 na sio miaka 15, kama askari mpelelezi anavyodai.

Awali, askari huyo mpelelezi Shaaban Nassor wa kituo cha Polisi Chake Chake kwenye shauri hilo, wakati akitoa ushahidi wake, alidai kuwa, kwa vielelezo alivyovipata vimethibitisha aliyebakwa na mshitakiwa huyo, ana umri wa miaka 15.

Alidai kuwa, kwanza alikabidhiwa cheti halisi cha kuzaliwa cha mtoto huyo na kisha katika kujiridhisha alimuhoji mama mzazi wa mtoto huyo, na kumueleza mwanawe kuwa ana umri wa miaka 15.

Askari huyo mpelelezi aliendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa, pamoja na cheti cha kuzaliwa na maelezo ya mama mzazi, alimpata daktari mtaalamu na vipimo vikaonesha kuwa mtoto yupo chini ya umri wa miaka 18, hivyo kwa sheria za Zanzibar bado ni mtoto.

“Mheshimiwa hakimu, mtoto aliyebakwa yuko chini ya miaka 18, na ndio maana nikamaliza upelelezi wangu na kisha jalada la kesi hiyo, kufikishwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa hatua za kisheria,’’alidai.

Mshatakiwa huyo, alipingana vikali na maelezo ya askari mpelelezi licha ya kutakiwa kumuuliza maswali, lakini alishikilia msimamo wake akidai kuwa, huyo sio mtoto tena.

Alidai kuwa, tayari mwaka huu amesha sherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa kutimiza miaka 20 ya kuzaliwa kwake.

“Iweje kama wewe askari mpelelezi, uiambie mahakama kuwa, niliyembaka ana miaka 15, wakati mwaka huu wa 2020 ameshafanya ‘birth day’ siku ya kuzaliwa na kutimiza miaka 20,’’alihoji mshitakiwa huyo.

Alisisitiza kuwa, sio mtoto na wala hajazaliwa mwaka 2003, kama alivyodai mpelelezi bali, alizaliwa Aprili 18, mwaka 2000 hasa kutokana na vitambulisho vyake mbali mbali, kikiwemo cha mzanzibari mkaazi.

Baada ya ombi hilo la mshtakiwa, hakim Luciano aliliahirisha shari hilo na kuliita tena Septemba 8, mwaka huu na kuutaka upande wa mashtaka kuwasilisha mashahidi waliobakia siku hiyo.

 Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Wakili wa serikali kutoka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka Juma Ali Juma kuwa, mshtakiwa huyo, alidaiwa kumbaka mtoto mwenye miaka 15.

Kufanya hivyo, ni kosa kinyume na kifungu cha 108 (1), (2) (e) na kifungu cha 109 (1) cha sheria ya Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar.