NA MARYAM SALUM, PEMBA

MAHAKAMA ya mkoa Chake Chake imemwachia huru mtuhumiwa Machano Haji Machano, mwenye miaka 20 aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya kwa madai kuwa, upelelezi wa shauri kutokwenda kwa mujibu wa sheria chini ya kifungu 142(1).

Kabla ya hakimu wa mahakama hiyo Luciano Makoye Nyengo, hajatoa hukumu hiyo, alimkumbushia mtuhumiwa huyo juu ya shauri lake linalomkabili.

Hakimu Luciano alidai kuwa sababu ambazo ziliifanya mahakama hiyo haukwenda kwa mujibu wa sheria ambapo mashahidi wawili waliohitajika kufika kwenye eneo la tukio hawakufika.

“Lakini pia kifungu cha 148(2) kilihitaji orodha ya vitu ambavyo vilipatikana katika upekuzi, ambapo sababu ya tatu pia hati ya hiyo ya orodha iwe imesainiwa na mashahidi kwani vitu vyote hivyo havikufanyika, na hati hiyo ya upekuzi haikuorodheshwa pia” alisema hakimu huyo.

Hakimu Luciano, alimalizia kutoa sababu za msingi ambazo ziliifanya mahakama kumwachia huru mtuhumiwa huyo kwamba hiyo sehemu iliyotuhumiwa kwamba dawa hizo yalipatakana kwenye zizi la kufungia ng’ombe, ambapo hakukuwa na ushahidi wala kuthibitishwa kuwa mmiliki wa eneo hilo ni la mshitakiwa ambavyo vitu hivyo vilipatikana.

Hakimu huyo alisema licha ya upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi sita kama ilivyokuwa upande wa utetezi, lakini bado shauri hilo liliandamwa na kasoro za kisheria na kuishawishi mahakama kumwachia huru mshitakiwa huyo.

  “Nikweli upande wa mashitaka uliwasilisha mashahidi wake akiwemo askari mpelelezi, lakini bado kulikuwa na kasoro za kisheria ndio maana mahakama hii imemwachia huru mtuhumiwa huyo,”alisema Luciano.

Pamoja na mtuhumiwa huyo, kuachiwa huru, lakini hakimu Luciano aliamuru kuwa dawa hizo za kulevya aina ya heroin na bangi ziteketezwe kisheria.