NA HAFSA GOLO
KATIBU wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kaskazini Kaskazini ‘B’ Unguja, Mula Othman Zubeir, amewataka wananchi wasifanye makosa katika kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura.
Alieleza hayo wakati alipokua akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Mahonda, ambapo alisema ushiriki wao katika uchaguzi ni hatua moja muhimu ambayo itawasaidia kutumia fursa ya kuchagua viongozi bora na wenye upeo wa kuitumikia nchi.
Mula alisema iwapo wananchi watatafakari na kufanya upembuzi bila ya shaka watawachagua viongozi ambao wataweza kuisaidia serikali katika suala la uimarishaji wa maendeleo na sio kuendeleza siasa za chuki na ubaguzi miongoni mwa jamii.
Alihimiza suala la wananchi kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kapeni za uchaguzi hasa za CCM kwani itasaidia kusiliza sera, ilani na mikakati ya kufikishiwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Sambamba na hilo,alisema ushiriki wao katika kampeni utasaidia kujenga maamuzi ya busara na hekma katika kuwachaguwa viongozi na sio kufuata mkumbo ama utashi wa kisiasa hasa vijana.
Akizungumzia kuhusu amani na utulivu,Mula alisema ili Zanzibar iendelee kuwa salama lazima watu wote waheshimu sheria na taratibu sambamba na kwenda kinyume na maadili ya uchaguzi.
Nae Katibu wa CCM Wilaya ya Kaskazini “B”,Mwansiti Hassan Mohamed, aliwataka vijana kuepuka kutumiwa vibaya na kushirikishwa katika vitendo vinavyochangia uvunjifu wa amani.