KHARTOUM, SUDAN

IDARA ya Ulinzi wa Raia nchini Sudan imetangaza kuongezeka kwa hasara zinazotokana na vifo vya watu na mali kutokana na mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo.

Kwa mujibu wa idara hiyo, zaidi ya watu 770,000 wamepata hasara kutokana na mafutiko hayo.

Televisheni ya RT imemnukuu Abdul Jalil Abur Rahim, Msemaji wa Baraza la Ulinzi wa Taifa wa Raia nchni Sudan akisema kwamba maeneo yaliyopata hasara kutokana na mafuriko hayo ni mengi, mashamba na ardhi za kilimo zimeharibiwa huku wafanyakazi wa misaada wakiendelea na juhudi zao uokozi na utoaji wa misaada kwa wahanga.

Wiki iliyopita, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilitangaza kuwa zaidi ya watu nusu milioni wa Sudan wameathiriwa na mafuriko makubwa yaliyotokea nchini humo kutokana na mvua kubwa zilizosababisha kujaa maji ya Mto Nile.

Taarifa iliyotolewa na OCHA ilisema kuwa, hadi Jumanne ya wiki iliyopita zaidi ya watu laki 500,000 walikuwa wameathirika na mafuriko nchini Sudan na kwamba maeneo ya Khartoum, kaskazini mwa Darfur na Sinar ndiyo yaliyopata hasara kubwa zaidi kutokana na mafuriko hayo.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa, mvua zinazoendelea kunyesha nchini Sudan zinatishia kuzuka maradhi ya kuambukiza na kukwamisha juhudi za kudhibiti maambukizi ya kirusi cha corona.