NA ASIA MWALIM

MWANAFUNZI wa darasa la tatu, skuli ya msingi Shauri moyo amefariki dunia baada ya kujinyonga, kwa kutumia kamba ya manila, ndani ya nyumba yao.

Kamanda wa Polisi Mkoa Mjini Magharibi Unguja (ACP) Awadh Juma Haji, aliyasema hayo alipokua akizungumza na waandishi wa habari huko Ofisini kwake Mwembemadema Mjini Zanzibar.

Kamanda Awadhi, alimtaja marehemu huyo alijulikana kwa jina la Yakub Yahya Khamis (10) mkaazi wa Mboriborini Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Alifahamisha kuwa tukio hilo lilifanyika Agosti 23 mwaka huu majira ya saa 02:15 asubuhi huko maeneo ya Mboriborini, ambapo mama mzazi wa marehemu akiwa kwenye shughuli zake za kawaida nyumbani kwake ndie aliebaini baada ya kumuona mwanawe akiwa ananinginia juu ya dirisha la ukumbini.

Aidha alisema kuwa marehemu alitumia dirisha hilo kwa kufunga kamba aina ya manila kwenye chuma kimoja cha dirisha hilo kwa kujinyonga na kupelekea kupoteza maisha.

Alisema kuwa baada ya tukio mwili wa marehemu ulifikishwa Hospitali ya Mnazi mmoja kwa uchunguzi wa kidaktari na baadae kukabidhiwa jamaa zake kwa ajili ya mazishi.

Kamanda Awadhi alisema Jeshi hilo lilifika eneo la tukio na kufanya uchunguzi wa tukio hilo, ambapo hawakufanikiwa kuona ujumbe wowote aliouacha marehemu wa kuonesha sababu za kufanya uamuzi huo.

Aidha Kamanda huyo aliwashauri wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao hasa wenye umri mdogo ili kuweza kujua matatizo yanayowakabili.

Alisema endeapo wazazi watawafatilia matatizo ya watoto wao kikamilifu, matukio mabaya kwa watoto yataweza kupungua, hivyo kuwapa ushauri unaofaa kutawarudisha katika hali zao za kawaida.