SIKU chache baada ya waziri mkuu wa Japan, Shinzo Abe kutangaza kujiuzulu nafasi hiyo kutokana na kuzorota kwa afya yake, chama tawala nchini humo cha Liberal Democratic, kimeanza harakati za kumsaka waziri mkuu mpya atakayechukua nafasi ya Abe.

Mnamo Agosti 28 mwaka huu, Abe alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo kwa kile alichokieleza kukabiliwa na hali mbaya ya kiafya hasa maradhi ya tumbo yanayomsumbua siku nyingi.

Taarifa za kitabibu zinaeleza kuwa waziri mkuu huyo anatatizo linalojulikana kama ‘Ulcerative colitis’, linalosababisha vidonda na uvimbe kwenye utumbo mpana, ambapo tatizo hilo la kiafya amekuwa nalo tangu alipokuwa kijana.

Abe aligundulika kurudiwa na maradhi hayo kufuatia vipimo mapema mwezi Julai mwaka huu wakati alipochunguzwa afya yake kwa wiki mbili mfululizo kwenye hospitali ya jijini Tokyo.

Katika hotuba yake ya kujiuzulu aliyoitoa, Abe alisema afya yake ilianza kudhoofika katikati ya mwezi Julai huu na alianza kusikia hali ya kuchoka, hata hivyo hakutaka hali hiyo iathiri maamuzi ya kisera.

“Nilitamani kupambana na ugonjwa huu na kutibiwa na sikuwa katika hali nzuri kabisa kiafya na bado nilitakiwa nifanye maamuzi muhimu ya kisiasa. Siwezi kufanya makosa yoyote, hasa katika kufanya maamuzi muhimu. Siwezi kufanya hivyo na niliamua kutoendelea na nafasi hii ya uwaziri mkuu”, alisema.

Hii ni mara ya pili kwa Abe kujiuzulu kwa sababu za matatizo ya kiafya, itakumbukwa kwamba mnamo mwaka 2007, alijiuzulu uwaziri mkuu kutokana na matatizo ya kiafya, mwaka mmoja tu baada ya kushinda uchaguzi mkuu.

Alirejea tena kwenye ulingo wa siasa baada ya kupata ahuweni na alishinda uchaguzi mwaka 2012, ambapo alitarajiwa kumaliza muhula wake madarakani hadi mwezi Septemba mwaka 2021.

Kutokana na kutokuwepo uwezekano wa Abe kurejea madarakani, chama tawala nchini humu cha Liberal Democratic kimeridhia kujiuzulu kwake, lakini pia kimeanza mchakato mara moja wa kumsaka mtu atakayechukua nafasi yake.

Mashauriano ya kutafuta waziri mkuu mpya wa Japan yameanza kukiwa kumesalia mwaka mmoja kabla ya kumalizika rasmi kipindi cha uongozi wa Abe.

Kwa mujibu wa katiba ya Japan, chama tawala cha Liberal Democratic ambacho kina viti vingi bungeni, kinayo haki ya kuchagua mmoja wa wanachama wake kushika nafasi ya waziri mkuu hadi wakati wa uchaguzi ujao mwezi Septemba mwaka 2021.

Kumejitokeza suali, nani anastahiki kuchukua nafasi ya Abe na kuwa waziri mkuu mpya wa Japan? Na serikali ya Abe na chama cha Liberal Democratic imepata mafanikia kiasi gani ya kukiwezesha kushinda tena katika uchaguzi ujao wa bunge?

Vyombo vya habari vya Japan vinataja majina ya wanasiasa watano wenye nafasi nzuri zaidi ya kushika nafasi iliyoachwa wazi na waziri mkuu huyo.

Mtu wa kwanza anayetajwa ni Tarō Asō, mwanasiasa mwenye umri wa miaka 79 ambaye tangu mwaka 2012 hadi sasa ameshika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo wizara ya uchumi, wizara ya fedha na naibu waziri mkuu wa Japan.

Nchini Japan Kōno anatambuliwa kuwa ni mwanasiasa mwanamageuzi ndani ya chama cha Liberal Democratic.

Wa pili ni Yoshihide Suga ambaye anatajwa kuwa na nafasi kubwa ya kushika nafasi ya uwaziri mkuu wa Japan. Itakumbukwa kwamba Suga ni miongoni mwa washauri waaminifu sana kwa Abe katika miaka kadhaa ya hivi karibuni.

Suga aliwahi kukana kuwa na nia ya kutaka kukalia kiti hicho, lakini alivutia shauku kutokana na mahojiano aliyoyafanya na shirika la habari la reuters na mashirika mengine kabla ya Abe kutangaza kujiuzulu.

Suga ambaye kwa sasa ni katibu mkuu wa baraza la mawaziri la Japan, aliamua kujiunga na mbio za kuwania kuwa kiongozi wa LDP akisema anapaswa kuchukua jukumu la mbele kutokana na matarajio ya uwezo wake wa kushughulikia matatizo.

Suga amekuwa na mchango mkubwa katika siasa za Japan kwenye muongo mmoja uliopita na alimrejesha madarakani tena Abe baada ya kipigo cha kihistoria katika uchaguzi wa mwaka 2007.

Wakosoaji wa serikali ya Japan wanasema kuwa, katika kipindi cha karibu miaka minane iliyopita ya uongozi wake, Shinzo Abe hakuwa na mafanikio makubwa yanayoweza kuandikwa katika historia ya nchi hiyo.

Mtu mwingine anayetazamiwa kushika nafasi iliyoachwa wazi na Abe ni mtaalamu wa masuala ya kijeshi, Shigeru Ishiba. Ishiba, kama alivyo Shizo Abe, ni miongoni mwa waungaji mkono wa suala la kuimarishwa zaidi uwezo wa kiulinzi wa Japan.

Waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje wa Japan, Fumio Kishida anashika nafasi ya tano kati ya wanasiasa wanaotajwa kuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo.

Waziri wa zamani wa mambo ya ndani Seiko Noda na waziri wa zamani wa ulinzi Tomomi Inada, ambaye anafahamika  kuwa mpenzi mno wa masuala ya bajeti, wanania  ya  kutaka  kuwa wanawake wa kwanza  nchini  Japan  kuwa  mawaziri  wakuu.

Waziri wa mazingira Shinjiro Koizumi, mwenye umri wa  miaka 39, mtoto  wa  waziri  mkuu  wa  zamani  Junichiro Koizumi  naye  anayefikiriwa  kuwa  waziri  mkuu  wa nchi hiyo.

Hata hivyo, Koizumi hatoshiriki katika mbio za sawa za uwaziri mkuu, lakini duru za kisiasa nchini humo zinaeleza kuwa ana mkono waziri wa ulinzi Taro Kono, iwapo atajiunga na  mbio  hizo.