NA MWAJUMA JUMA

LIGI daraja la pili Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja imemalizika na timu ya Gulioni FC kutwaa ubingwa.

Ligi hiyo ilikuwa ilishirikisha timu 14 ambazo zinatoka katika wilaya tatu za Mkoa huo,ambazo ni wilaya ya Mjini, Magharibi  A na B.

Kwa vile ligi hiyo imemalizika na bingwa kupatikana na msimu ujao itashiriki ligi daraja la kwanza Kanda ya Unguja.

Hivyo basi  nachukua fursa hii kuwapongeza Gulioni FC kwa kufanikiwa kutwaa ubingwa na kupanda daraja, lakini pia nitoe rai yangu kwa timu hiyo.

Jambo kubwa ambalo nataka kuwaambia Gulioni ni kuhakikisha wanajiandaa mapema, ili kuhakikisha inafanya vyema kinyume chake itajikuta inarudi ilikotoka.

Ni ukweli usio na kificho hata kidogo kuwa daraja ambalo timu hiyo imepanda ni tofauti na kule walikotoka, kwani hatua hiyo mpya ambayo wanakwenda kukumbana nayo ni ngumu sana kulinganisha na walikokuwa wakicheza.

Miongoni mwa maandalizi ambayo wanatakiwa kuyafanya moja wapo ni kufanya usajili mzuri kwa kuchagua wachezaji Ambao watawasaidia katika kupeleka mbele timu hiyo,ambao wana viwango vizuri na kwa hapa Zanzibar wapo wengi sana.

Gulioni inatakiwa kutambua kwamba daraja ambalo wanakwenda kushiriki ni kubwa na linaundwa na timu zenye uwezo mkubwa na wazoefu.

Hivyo wanapaswa kukaa na  kupanga mipango mizuri ambayo kwa namna moja au nyingine itawasaidia kufikia malengo yao, badala ya kujikuta wanarudi nyuma walikotoka.

Ni vyema basi wakafahamu kwa kina kuwa kupanda daraja ni   kitu chengine lakini kinachofuata ni maandalizi mazuri, ili kuweza kufikia malengo yao kama ambavyo walifanya wakati wa kutaka kupandisha timu.

Hivyo ushirikiano ambao mlionyesha wakati ligi daraja la pili mnapaswa kuuzidisha zaidi na kuendelezwa kwa maslahi ya  timu yao.

Pia wanapashwa kutambua kuwa chuki, uhasama majungu na mambo mengine mengi ambayo yatawaharibia mipango yao, si vyema kupewa nafasi kwenye timu katika kipindi ambacho wanaelekea kucheza daraja jipya.

Tumekuwa tukishuhudia mara nyingi timu ambazo hupanda daraja, badala ya kujiimarisha hujikuta wanafanya ,mambo ya ajabu na kudumaza maendeleo yao.

Kwa minajili hiyo ni lazima viongozi wajipange na kuhakikisha yote ambayo wanayafanya yawe wameyafanya kwa pamoja ili kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima.

Hivyo Gulioni ikumbuke kuwa katika daraja hilo kuna kazi kubwa ambayo kama hawatakuwa makini, watajikuta wanashindwa kutimiza malengo yao ambayo wamejiwekea.

Nafahamu kuwa wakati wa usajili ni lazima kuna  baadhi ya wachezaji wataachwa na wengine watabakia, hivyo kwa wale ambao wataachwa wasione kuwa wameonewa na kuanza kutia sumu mbaya kwa wengine.

Nawatakia kila la kheri katika msimu wao mpya wa ligi daraja la Kwanza Kanda ya Unguja ya 2020/2021.