MNAMO Agosti 20, kulisambaa taarifa za kulishwa sumu akiwa kwenye ndege kwa mmoja wa wapinzani wakubwa wa rais wa Urusi Vladimir Putin, Alexei Navalny.

Muda mfupi baada ya Navalny kulishwa sumu, alipelekwa hospitali na kuwekwa kwenye wodi ya wagonjwa mahututi kiasi cha kutotambua nini kinaendelea duniani huku akisaidia kupumua na mashine.

Navalny, alikumbwa na mkasa wa kulishwa sumu kiasi cha hivi sasa kupigania uhai wake alipokuwa akisafiri kwa ndege akisafiri kuelekea mjini Moscow kutoka mji wa Tomsk ulioko Siberia.

Kira Yarmysh msemaji wa mpinzani huyo wa Putin, alikuwa wa kwanza kueleza kilichomfika Navalny, ambapo alisema alisema yuko katika hali mahututi na alikuwa akitokwa jasho jingi akiwa kwenye ndege na alimuomba amzungumzishe ili aweze kuendelea kuwa na fahamu ya kinachoendelea na baadae alikwenda msalani na kuzimia.

Yarmysh akaongeza kusema kwamba mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 44 ni lazima alikunywa kitu kilichotiwa ndani ya chai aliyokunywa mapema asubuhi alipokuwa katika mgahawa mmoja kwenye uwanja wa ndege kabla ya kupanda ndege hiyo.

Ujumbe alioutoa msemaji wa mwanasiasa huyo mkosoaji wa rais Putin ameeleza kwamba madaktari wanasema sumu iliingia haraka kwenye mwili kutokana na kinywaji cha moto.

Siku chache baadae, Navalny alilamzimika kusafirishwa kupelekwa nchini Ujerumani ili kupata matibabu zaidi, ambako akiwa nchini huko pia alifanyiwa vipimo upya.

Kwa mujibu wa madaktari kutoka nchini Ujerumani, walieleza kuwa kuna ushahidi unaoonesha kwamba Navalny alipewa sumu ya Novichok inayoathiri neva.

Alexei Navalny ni nani? Alijipatia umaaru kwa kufichua vitendo vya rushwa akikitaja chama cha Putin cha United Russia kuwa ni chama cha wezi na wahalifu na alitumikia vifungo kadhaa gerezani.

Mwaka 2011 alikamatwa na kufungwa kwa siku 15 baada ya maandamano yaliyodai kuwepo kwa vitendo vya wizi wa kura vilivyodaiwa kufanywa na chama tawala katika kura za ubunge.

Navalny alitumikia kifungo mwezi Julai mwaka 2013 kwa makosa ya matumizi mabaya ya fedha, lakini alisema kuwa hukumu hiyo ilichochewa kisiasa. Alijaribu kusimama kuwania nafasi ya urais mwaka 2018, lakini alizuiwa kwa kuwa alikuwa tayari amehukumiwa kifungo.

Navalny alifungwa siku 30 gerezani mwezi Julai mwaka 2019 kwa kosa la kuitisha maandamano ambayo yalikuwa batili.

Jina Novichok linamaanisha “mgeni” Kirusi, na ni la sumu kali iliyotengenezwa na uliokuwa Umoja wa Kisovieti miaka ya 1970 na 1980.

Sumu ya Novichok ina athari sawa na sumu zingine, inafanya kazi kwa kufunga mawasiliano kutoka kwenye neva hadi kwenye misuli na kufanya viungo vingi kushindwa kufanya kazi.

Ikiwa baadhi ya sumu hiyo ni ya majimaji, inaaminika kuna nyingine za vidonge. Hii ikimaanisha kwamba inaweza kutawanywa kama ungaunga.

Sumu ya Novichocks imetengenzwa kuwa na sumu zaidi kuliko silaha za kemikali na hivyo basi baadhi ya sumu hiyo hufanya kazi haraka sana mwilini kati ya sekunde 30 hadi dakika mbili.

Nani mwingine aliyewahi kutiliwa sumu hiyo? mwaka 2006, Alexander Litvinenko aliyekuwa ofisa wa kijasusi wa Urusi ambaye aligeuka na kuwa mkosoaji wa Urusi na kukimbilia Uingereza, alifariki dunia baada ya chai yake kutiliwa sumu aina ya polonium-210.

Mwaka 2018, Sergei Skripal na binti yake Yulia walikuwa katika hali mbaya sana katika mji wa Uingereza wa Salisbury, baada ya washukiwa wawili wa Urusi kusemekana kwamba wamewanyunyizia sumu hiyo kwenye kishikio cha mlango katika nyumba ya Skripal, aliyekuwa jasusi wa Urusi.

Hivi karibuni, wanahabari na mwanaharakati wa upinzani Vladimir Kara-Murza inasemekana kwamba alitiliwa sumu mara mbili na vikosi vya usalama Urusi, nusra afariki dunia baada kupata matatizo ya figo mwaka 2015 na miaka miwili baadae alipoteza fahamu kwa wiki moja.

Mkosoaji mwingine wa Kremlin, Pyotr Verzilov, aliishutumu idara ya ujasusi ya Urusi kwa kumtilia sumu mwaka 2018, alipougua baada ya kusikilizwa kwa kesi, na akapoteza uwezo wake wa kuona na kuzungumza.

Viongozi kutoka kote ulimwenguni wamelaani tukio la kupewa sumu kiongozi wa upinzani Urusi Alexei Navalny katika jaribio la kutaka kumuuwa. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema anatarajia Urusi kueleza msimamo wake.

Merkel alisema kulikuwa na “habari za kutisha” zilizoonesha “bila shaka yoyote” kuwa tukio la kupewa sumu Alexei Navalny lilikuwa “jaribio la mauaji kwa kutumia sumu inayoathiri mishipa ya fahamu.

Merkel alisema Navalny ni “muhanga wa uhalifu ulionuia kumnyamazisha,” akiongeza kuwa ukubwa wa suala hilo ni muhimu kwake “kuchukua msimamo wa wazi”.

Hatima ya Alexei Navalny imevutia hisia za ulimwengu wote. Ulimwengu utasubiri majibu na kueleza kuwa “Tutawafahamisha washirika wetu wa EU na NATO kuhusu matokeo haya ya uchunguzi”.

“Tutashauriana na kuamua hatua mwafaka ya pamoja tutakayochukua kwa kutegemea na kuhusika kwa Urusi. Uhalifu dhidi ya Alexei Navalny ni kinyume na maadili na haki za msingi tunazozilinda”.

Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani John Ullyot amesema kitendo hicho ni cha kukemewa kabisa na kuwa watashirikiana na washirika ili kuwawajibisha waliohusika nchini Urusi.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amesema amefadhaishwa na ufichuzi huo na akalaani matumizi ya bila kujali ya sumu ya aina hiyo.

Jumuiya ya Kujihami ya NATO imesema Urusi lazima ifanye uchunguzi kamili na wa uwazi. Katibu Mkuu Jens Stolltenberg amesema NATO itashauriana na Ujerumani na washirika wake wote kuhusu hatua za kuchukua.