BERLIN, UJERUMANI

MWANASIASA wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny anayeshukiwa kuwekewa sumu inayoathiri mfumo wa neva ameruhusiwa kuondoka Hospitalini.

Navalny ambaye ni mkosoaji wa Rais Vladimir Putin alipoteza fahamu akiwa safarini kwenye ndege nchini Urusi mwezi Agosti mwaka huu.

Mwanasiasa huyo alikua  akitibiwa katika Hospitali moja nchini Ujerumani alikosafirishwa kwa ndege.

Hospitali hiyo ilitoa taarifa,ikisema mwanasiasa huyo aliruhusiwa kuondoka siku iliyotangulia.

Navalny mwenyewe aliweka ujumbe mtandaoni  uliosema kuwa atapewa tiba ya kumfanya arejee maisha yake ya kawaida kwani hawezi kusimama kwa mguu mmoja au kurusha mpira kwa kutumia mkono wake wa kushoto.

Mnamo Septemba 15,msemaji wake alifichua kuwepo uwezekano wa mipango ya kurejea nchini Urusi.

Wafuasi wa Navalny walielezea wasiwasi wao kwamba maisha yake huenda yakawa hatarini ikiwa atarejea nchini Urusi.