NA MARYAM HASSAN

ALIYEIBA nazi 18 zenye thamani ya shilingi 10,000 amepelekwa rumande baada ya kushindwa kujidhamini bondi ya shilingi 20,000.

Mshitakiwa huyo ni Richard Daudi Richard (20) mkaazi wa Tunguu ambae alifikishwa mahakamani hapo kwa kosa la wizi wa mazao.

Richard alitakiwa kujidhamini kima hicho huku akitakiwa kuwasilisha wadhamini wawili ambao anao wasaini kima hicho pamoja na kuwasilisha barua ya Sheha na kopi ya kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, masharti ambayo yalimshinda.

Hatua ya kutaka kujidhamini kiasi hicho imekuja baada ya mshitakiwa huyo kuomba kupewa dhamana mbele ya Hakimu wa Mahakama ya wilaya Mwera Taki Abdalla Habibu.

Hati ya mshitakiwa huyo ilisomwa na wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Safia Serembe, kwamba mshitakiwa alitenda kosa hilo Disemba 2, mwaka 2018, majira ya 3:00 za asubuhi huko Tunguu  kwa Shemego Wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Ambapo bila ya halali na kwa dai la udanganyifu mshitakiwa huyo aliiba nazi 18 zilizokuwa hazijafuliwa zenye thamani ya shilingi 10,000 mali ya Nassor Salum Baesh, jambo ambalo ni kosa kisheria.