NA HUSNA SHEHA

MGAZA Hassan Rehani (23) mkaazi wa Mahonda Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya Mahonda akikabiliwa na kosa la wizi wa Nazi.

Mshitakiwa huyo alisomewa shitaka lake na Mwendesha Mashitaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka  DPP Ali Juma mbele ya Hakimu Nyange Makame Ali .

Mshitakiwa huyo alidaiwa kuiba nazi saba zenye thamani ya shilingi 7,000 kwa makisio mali Jumanne Hassan Kanyerese ,jambo ambalo ni kosa kisheria.

Mshitakiwa huyo alidaiwa kufanya wizi huo Agosti 27 mwaka huu majira ya saa 10:00 jioni huko Mahonda Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Upande huo wa mashitaka uliwasilisha nazi hizo ambazo hazijafuliwa zikiwa mbili za mnazi mwekundu na tano mweusi, ni kielelezo cha kesi hiyo. 

Baada ya kusomewa shitaka lake mshitakiwa alikataa kosa na kuiomba Mahakama impatie dhamana ombi ambalo halikua pingamizi kwa pande zote mbili.

Hata hivyo upande wa Mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo tayari umeshakalimika na kuomba tarehe nyengine kwa kusikiliza ushahidi.

Mshitakiwa huyo anatarajiwa kupandishwa tena Mahakamani hapo Septemba 14 mwaka huu kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi,akiwa yupo nje kwa dhamana ya maandishi ya shilingi 100,000 na kuwasilisha kopi ya kitambulisho cha Mzanzibar pamoja na barua ya sheha wa shehia wanazoishi kila mmoja.