NA KHAMISUU ABDALLAH
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa ameitaka Benki ya NCBA kubuni njia mbalimbali za mapato katika huduma watakazotoa ili kuingia katika soko la ushindani wa biashara za kibenki.
Kauli hiyo aliitoa katika hafla ya kuzindua tawi jipya la benki hiyo huko Mlandege mjini Zanzibar.
Alisema, hatua hiyo itasaidia kuwavutia wateja na kuweza kufikia malengo waliyojiwekea kwenye kuongeza mapato.
Balozi Ramia, alisema serikali inashirikiana na mabenki mbalimjbali kwenye sekta ya kibenki ili ziweze kufanya shughuli zao ipasavyo na kukuza uchumi wa nchi.
Hata hivyo, alibainisha kuwa ufunguaji wa matawi ya kibenki nchini unatoa fursa mbalimbali kwa wawekezaji na wafanyabiashara hapa nchini.
“Kuongezeka kwa huduma za kibenki nchini ni kuendelea kukua kwa fursa za kiuchumi na kuimarisha huduma hizi kwa wananchi wetu wa ndani na nje”, alisema.
Hivyo, aliyataka makampuni ya kibenki kuangalia upya uwekezaji wa matawi katika maeneo ya vijijini ili kuona wananchi wa maeneo hayo nao wananufaika na huduma hizo.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo Margeti Karume, alisema benki hiyo ipo kwa ajili ya kurahisisha huduma za kibenki kwa wananchi kwa urahisi zaidi.
Aliwahakikishia wananchi kuwa benki hiyo ipo makini kwenye utoaji wa huduma zake na tayari ina wateja millioni 150 katika matawi mbalimbali hapa nchini ikiwemo Uganda na Tanzania bara. Hivyo, aliwaomba wananchi kutumia fursa za benki hiyo ili kunufaika na huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo.