NA JOSEPH NGILISHO, ARUSHA

TUME ya  uchaguzi nchini imewaonya  wagombea wanaojitangaza  kwa wananchi kuwa tayari wameshashinda  katika uchaguzi huu wakati Bado  uchaguzi haujafanyika na hivyo kuleta taharuki kwa wananchi ambao ndio wapiga kura.

Akizungumza  jana jijini Arusha Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi  nchini NEC, Dk. Charles Mahera, amesema kuwa tume ya uchaguzi  ndio yenye   mamlaka  kisheria ya kutangaza matokeo  ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na siku ya uchaguzi bado  hivyo Tume imewaonya wagombea kuacha kupotosha  watanzania na kuwajengea taswira kuwa wamekwisha shinda .

Amesema kitendo hicho ni kibaya kwani kunakuwa na malengo ya kuvuruga  amani kwa watanzania na nikinyume na taratibu za sheria hivyo kitendo kinachofanywa na baadhi ya wagombea kwa kuikashifu tume ya uchaguzi kuwa itaiba kura  ni kuidhalilisha na kuitisha  tume isifanye kazi yake .

” Wagombea wa aina hiyo wanapaswa kupuuzwa na watanzania kwani hali hiyo ni moja ya dalili ya uoga anajihami au amekosa sera zakuwaeleza wananchi  hivyo hafai kusikilizwa,”amesema Mahera.

Kwa kitendo hicho tume ya maadili taifa  imemwandikia barua ya wito Mgombea Urais was CHADEMA, Tundu Lisu, ya kwenda kueleza alichokisema katika kampeni zake alipokuwa mkoani Musoma juzi tarehe 26  hivyo barua hiyo inamtaka aende leo.

Hata hivyo Dk. Mahera amesema kuwa  tangu Septemba   25, 2020, Mkurugenzi wa uchaguzi watume ya uchaguzi anaendelea na ziara ya kukagua na kuratibu maandalizi ya uchaguzi katika majimbo ya mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro kuhakikisha vifaa vya uchaguzi Kama vimefika katika maeneo husika.