NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imevitaka vyombo vya habari nchini kuwa makini kwa kuhakikisha kuwa haviwi chanzo cha kutokea mtafaruku katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu.

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk. Wilson Mahera Charles alieleza hayo wakati akifungua semina ya siku moja kwa watoa huduma ya habari mitandaoni iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano ya Kimataifa ya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Alisema wakati huu ni muhimu sana kwa vyombo vya habari kuhakikisha vinazingatia maadili ya taaluma zao hali ambayo itaongeza utulivu miongoni mwa wananchi.

Aliongeza kusema kwamba, katika kipindi cha kampeni vyama vya siasa vinapata fursa ya kuwanadi wagombea na kuelezea sera na ilani za uchaguzi za vyama vyao, hivyo uzoefu unaonyesha kuwa kipindi hiki kunakuwa na joto la kisiasa linalotokana na baadhi ya watu kukosa uvumilivu.

Alieleza kuwa kampeni zinasimamiwa na maadili ya uchaguzi, hivyo Tume kwa kushirikiana na vyama waliandaa maadili ambayo yalisainiwa pande zote mnamo Mei 27 mwaka huu.

Alifafanua kuwa, maadili ya uchaguzi na mambo mengine yanavitaka vyama kufanya kampeni za kistaarabu na kuepuka kufanya fujo au kuchochea vurugu ya aina yeyote katika mikutano ya vyama vingine kwa kutokutumia lugha ya matusi kashfa, kejeli, udhalilishaji na vitisho au lugha inayochochea uvunjifu wa amani.

Aidha alisema kipindi hiki kitumike kuwahamasisha wananchi hasa wapiga kura kushiriki katika kampeni hizo ili waweze kuwapima wagombea na hatimae kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.

Akigusia rufaa alisema zinaendelea kushughulikiwa zote zilizofikishwa kwao na majibu ya sheria na taratibu za uchaguzi na sio shindikizo la mtu au taasisi ama chama zitatolewa majibu.

Naye Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Aisha Omar aliwataka watoa huduma ya habari mitandaoni kufanya kazi zao kwa weledi kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.