NA MWANDISHI WETU
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekutana na asasi za kiraia ambazo zimepata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura ili kuisadia jamii kujua haki yao ya kuchagua viongozi wawatakao katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu.
Akifungua mkutano huo Maisara jana, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura, Giveness Aswile alizitaka taasisi hizo kujikita kwenye elimu ya mpiga kura na kuvitumia vibali walivyopewa kama ilivyokusudiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Aliwataka wawakilishi wa asasi hizo kutochanganya elimu ya mpiga kura na kampeni za vyama vya siasa na kutoegemea upande wowote katika utoaji wa elimu.
Aidha aliwataka kuwa makini na mambo ambayo yanaweza kuleta sintofahamu bila sababu yoyote ya msingi katika utoaji wa elimu hiyo.“Mmepewa maelekezo ya kutotumia kwa ubia vibali mlivyopewa na Tume na asasi nyengine yoyote ile hasa zile ambazo hazijapata vibali,”alisema.
Alieleza kuwa Tume inafahamu kuwa baadhi ya asasi zilizopewa vibali wakati wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura,zilitumia vibali vyao kwa ubia na asasi nyingine, hata hivyo hatarajii kwa asasi zilizopewa vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura kuwa vinaweza kufanya hivyo.
Alisema kwa asasi ambazo zilibainika kufanya hivyo ni moja wapo ya sababu ya baadhi yao kunyimwa vibali vya kutoa elimu hiyo.
“Tume inaendelea na itaendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu, asasi yoyote itakayobainika kukiuka maagizo na maelekezo mliyopewa,Tume haitasita kusitisha kibali wakati wowote,”alisema.