NA MWAJUMA JUMA

TIMU ya soka ya New Generation imeanza vyema ligi kuu ya Zanzibar ya soka la wanawake kwa ushindi mnono wa mabao 15-0 dhidi ya Green Queens.

Mchezo huo ambao ni wa ufunguzi ulichezwa kwenye uwanja Mao Zedong majira ya saa 10:00 za jioni.

New Generation ambao mastakimu yao yapo Kwahani walijipatia mabao yao hayo kupitia Zamoyonce James na Warda Abdulhakim ambao walifunga mabao matatu kila mmoja.

Wengine ni Hawa Faraham, Hafidha Juma na Maimuna Khamis ambao walifunga mabao mawili mawili, huku Hawa Ali Juma, Riziki Abubakar na Mwajuma Abdalla wakafunga bao moja kila mmoja.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena Jumamosi ya Septemba 19 mwaka huu,  kwa mchezo mmoja ambao utawakutanisha Jumbi Queens na Kidimni, ambao utachezwa kwenye uwanja wa Mao Zedong saa 10:00 za jioni.