NA MWAJUMA JUMA
TIMU ya soka ya New Kingi imo katika maandalizi kabambe kwa ajili ya kujiandaa na ligi daraja la pili Mkoa wa Kaskazini Unguja hatua ya nne bora ambayo itaanza hivi karibuni.
Kocha wa timu hiyo Ame Dunia alimwambia mwandishi wa habari hizi kwamba mpaka sasa timu yao inaendelea kufanya mazoezi kama kawaida ikiwemo kucheza mechi za kirafiki ili kuzidi kujiweka sawa.
New Kingi ambayo mastakimu yake ipo Kinyasini Unguja imefikia hatua hiyo, baada ya kushika nafasi ya kwanza kwenye kundi lake A akiwa na pointi 34.
Alisema bado timu yao ina mpango wa kupanda daraja na ndio maana pamoja na kuwa ligi ya makundi imekwisha lakini bado wanaendelea na mazoezi kama kawaida.
Hata hivyo alisema wana mpango wa kucheza mechi nyingi za kirafiki na timu za ligi kuu kama ligi hiyo itachelewa kuanza.
Ligi hiyo ya nne bora ya mkoa huo inashirikisha timu za New King, coast United, Kitope United na Black Mamba.