MPINZANI mkubwa wa rais wa Urusi, Alexei Navalnya anaendelea kupatiwa matibabu kwa kile kinachodaiwa kuwa lililishwa sumu ya moja wapo ya aina za ‘novichok’, inayosemakana ni sumu hatari sana.

Madaktari katika hospitali ya Charite iliyopo mjini Berlin nchini Ujerumani ndio waliothibitisha kwamba Navalny alipewa sumu, huku wakibainisha kuwa kuwa mpinzani huyo Vladimir Putin atachukua muda kupona.

Si mara ya kwanza Urusi kudaiwa kutumia sumu ya ‘novichok’ katika kujaribu kuwafumba midomo wapinzani, ambapo itakumbukwa kuwa mnamo mwaka 2018, zilikuwepo taarifa kwamba Urusi ilitaka kumuua, Sergei Skripal pamoja na binti yake Yulia kwa kutumia simu ya aina hiyo.

Taarifa zilieleza kuwa Skripal na binti yake walipewa sumu kufuatia Urusi kuwatuhumu kuvujisha taarifa za kijasusi za Urusi kwa mataifa ya kigeni.

Kwa sasa shirika la kudhibiti matumizi ya silaha za sumu (OPCW) limeelezea wasiwasi mkubwa baada ya Ujerumani kueleza kuwa Navalny alipewa sumu aina ya ‘novichok’, inayoua mishipa ya fahamu.

Katika makala haya tuiangalie japo kwa ufupi sana sumu ya ‘novichok’ambayo inachukuliwa kama miongoni mwa silaha za sumu.

Sumu ya jamii za ‘novichok’, ziliundwa kwa uliokuwa muungano wa nchi za Usovieti na maana ya neno ‘novichok’ kwa lugha ya kirusi ni mgeni.

‘Novichok’ ni jina linalotumiwa kurejelea kemikali za sumu ambazo hushambulia mfumo wa neva mwilini, kemikali hizo zilitengenezwa baina ya mwaka 1970 na 1980.

Jamii ya sumu za ‘novichok’ zilifahamika kama silaha za kemikali za kizazi cha nne na zilistawishwa chini ya mpango wa silaha za muungano wa Usovieti uliofahamika kama “Foliant”.

Mnamo mwaka 1999, maofisa wa ulinzi kutoka Marekani walisafiri hadi Uzbekistan kusaidia kuvunja na kusafisha moja ya eneo kubwa zaidi lililotumiwa kufanyia majaribio silaha za kemikali la uliokuwa muungano wa Usovieti.

Kwa mujibu wa ofisa mmoja wa ngazi za juu ambaye alitorokea Marekani, maofisa wa Usovieti walitumia kiwanda kilichokuwa eneo hilo kuunda na kufanyia majaribio sampuli za kemikali ya sumu za ‘novichok’.

Kemikali hiyo iliundwa mahsusi kutoweza kugunduliwa na wakaguzi wa silaha na sumu katika mataifa mengine, ambapo inaelezwa kuwa ni sumu yenye nguvu kuliko sumu nyingine.

Moja ya kemikali hizi zinazofahamika kama sumu ya ‘novichok’ – A-230 – inadaiwa kuwa na nguvu mara 5-8 zaidi ya sumu nyingine hatari kwa jina VX.

“Hii ni sumu hatari na changamano kushinda sumu aina ya sarin au VX na pia huwa vigumu zaidi kuitambua,” anasema Prof. Gary Stephens, mtaalamu wa kemikali katika Chuo Kikuu cha Reading kilichopo nchini Uingereza.

Taarifa zinaeleza kuwa sumu aina ya VX ndiyo iliyotumiwa kumuua ndugu wa kambo wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un mwaka miacka michake iliyopita, taarifa hii ni kwa mujibu wa uchunguzi wa Marekani.

Aina mbalimbali za kemikali hii ya A-230 zimekuwa zikitengenezwa, na aina moja inadaiwa kuidhinishwa na jeshi la Urusi itumike kama silaha ya kemikali.

Kuna aina mbalimbali za sumu ya ‘novichok’, ingawa baadhi ya aina za sumu hiyo huwa majimaji, pia kuna aina nyingine ambazo ni yabisi (ngumu au isiyokuwa majimaji), sumu ya ‘novichok’inaweza kugeuzwa kuwa poda laini.

Baadhi ya sumu hizi pia hudaiwa kutumiwa kama silaha za ngazi mbili. Hii ina maana kwamba sumu hiyo huhifadhiwa mara nyingi kama kemikali aina mbili ambazo zikiwa kando kando si hatari.

Zinapochanganywa, huingiliana na kutengeneza sumu. Hii huifanya rahisi sana kwa viungo vya kemikali hii kusafirishwa kwani huwa sumu tu zikichanganywa.

“Moja ya sababu ambayo hufanya sumu hizi kuandaliwa ni kwa sababu viungo vyenyewe havijapigwa marufuku,” anasema Prof. Stephens.

“Hii ina maana kwamba kemikali hizi ambazo huchanganywa huwa rahisi sana kusafirishwa bila kuwa hatari kwa anayezisafirisha.”

Kwa mujibu wa utaifi sumu aina ya ‘novichok’ zinaweza kumuathiri mtu kwa haraka sana. Ikitokea mtu anapovuta sumu ya ‘novichok’, au hata ikigusa ngozi yake, basi huanza kumuathiri haraka sana.

Dalili zake zinaweza kuanza kujionesha katika kipindi cha muda mfupi hivi, sekunde 30 hadi dakika mbili. Hata hivyo, sumu hii ikiwa kama poda huchukua muda zaidi kuanza kuathiri mtu.

Dalili kali zinaweza kuanza kujionesha saa 18 baada ya mtu kukumbana na sumu hiyo, ambapo huathiri mfumo wa mshipa ya fahamu (neva). Sumu aina ya ‘novichok’ huwa na madhara sawa na ya sumu nyingine zenye kushambuliwa mfumo wa neva.

Hii ina maana kwamba huwa zinafanya kazi kwa kuzuia ujumbe au mawasiliano kati ya mfumo wa neva na misuli na pia kusambaratisha shughuli nyingi muhimu za mifumo mwilini.

Dalili zake ni pamoja na macho kuwa na rangi nyeupe, huku mboni za macho zikiminyika, viungo kunyong’onyea na mtu kuonekana kupumbaa, wakati mwingine, mtu hupoteza fahamu, kushindwa na kupumua na kufa.

Sumu hizi kimsingi hufanya moyo kupunguza mapigo yake na kubana njia zinazotumiwa na mwili kupumua na mwishowe mtu kufariki kutokana na mtu kukosa hewa ya kutosha.

Baadhi ya aina za sumu hii ya ‘novichok’ zimeundwa mahsusi kuhakikisha dawa za kawaida za kupoza nguvu ya sumu haziwezi kufanikiwa.

Iwapo mtu amepewa sumu, anapaswa kuvuliwa mavazi yake na ngozi yake kuoshwa vyema kwa maji na sabuni. Macho yake yanafaa pia kuoshwa vyema kwa maji na apewe hewa ya oksijeni.