NA MADINA ISSA
OFISI ya Mufti Zanzibar, imesema itaendeleza jukumu la kusimamia mafunzo ya ndoa ili kuweza kuepusha migogoro katika ndoa pamoja na wimbi la talaka.
Katibu wa Mufti wa Zanzibar, shehe, Khalid Ali Mfaume, aliyasema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya ndoa kwa mkupuo wa saba yaliyofanyika katika msikiti wa Zinjibar uliopo Kimbesamaki Mjini Unguja.
Alisema kuwa hivi sasa katika ndoa kumekuwepo na migogoro isiyokwisha na talaka sizizo na sababu maalum na kupelekea kukosekana na utulivu katika ndoa.
Aidha alisema kuwa serikali imeipa jukumu la kuweza kusimamia na kupunguza wimbi la takala na kuiwezesha ofisi hiyo kuendelea kutoa mafunzo ya ndoa, ili kuweza kuzinusuru ndoa pamoja na kuepusha migogoro yanayotokezea baina ya wanandoa.
Alisema vijana wengi wanapotaka kufunga ndoa huwa hawapatiwi mafunzo ya kutosha jambo ambalo linasababisha kujitokeza masuala mengi katika ndoa zao.
“Vijana wanaharakia kuolewa ama kuoa huwa hawapati mafunzo hasa jinsi ya kwenda kuishi katika familia waliyokubaliana hivyo, inapeleka kupata matatizo ikiwemo kuachwa na kuendeleza migogoro wakati wa ndoa” alisema.
Hivyo, aliwataka wanajamii wanaopatiwa mafunzo hayo, kuweza kuyasikiliza vizuri sambamba na kuyatekeleza kivitendo, ili kuweza kupata faida katika ndoa zao pamoja na kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza.
Nae Ofisa Utafiti na Taaluma Shehe, Abdul Simba Khamis, alisema kila kitu kinahitaji elimu, hivyo, ni vyema kwa anayetaka kufunga ndoa kuhakikisha anapata mafunzo ya kutosha, ili kuweza kufanya jambo kwa usahihi wakati wa ndoa.
Katika mafunzo hayo mada zitakazosomeshwa ni umuhimu wa ndoa, migogoro inayojitokeza katika ndoa, talaka na hikma zake, uzazi wa mpango, mirathi, kujua aina ya eda.