NAIROBI,KENYA

KATIBU Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wauguzi KNUN Seth Panyako ametoa wito kwa Umoja wa Matifa UN kuingilia kati suala la uchunguzi wa uporaji fedha zilizotengwa kukabili janga la Corona nchini humo.

Akizungumza wakati wa ibada mjini Kakamega,Panyako alisema suala la mawaziri na makatibu wa Wizara kuhusishwa katika uporaji wa fedha za umma ni hali ya kusikitisha hivyo kusisiza haja ya mashirika ya kimataifa kuingilila kati.

Panyako alitumia fursa hiyo kuunga mkono shinikizo la kumtaka Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kujiuzulu baada ya kuhusishwa na wizi wa fedha zilizotengwa kununua vifaa vya kukabili janga la Corona.

Wakati huo huo, alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kuwafuta kazi Waziri Kagwe pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Susan Mochache, baada ya kuhusishwa na wizi wa fedha zilizotengewa Mamlaka ya Usambazaji wa Vifaa vya Matibabu KEMSA.

Aidha, Panyako alizitaka idara za uchunguzi kuchunguza matumizi ya fedha katika kila kaunti ikiwemo Kakamega, ambayo inadaiwa kufuja zaidi ya shilingi milioni mia moja zilizofaa kutumika kukabili janga la corona.

Hayo yanajiri huku Mochache wiki ijayo akitarajiwa kufika kwa mara nyengine mbele ya kamati ya Seneti inayochunguza kashfa ya ufisadi katika Mamlaka ya KEMSA ili kujieleza hasa baada ya kuhusishwa pakubwa na uporaji huo.

Juzi Waziri Kagwe na Mochache walihusishwa pakubwa na sakata hiyo kufuatia kuhojiwa kwa Aliyekuwa Ofisa Mkuu Mtendaji  wa KEMSA aliyesimamishwa kazi Jonah Manjari  ambaye alidai kwamba alishinikizwa na Waziri Kagwe pamoja na Mochache kufanya baadhi ya maamuzi.

Akihojiwa na kamati ya Seneti, Manjari alisema alikuwa akiwasiliana na Waziri Kagwe na Mochache kupitia mawasiliano ya simu au ujumbe mfupi hatua iliyomfanya kununua baadhi ya vifaa bila kufuata sheria za ununuzi.