NA SAIDA ISSA, DODOMA
BENKI ya watu wa Zanzibar (PBZ) kwa kushirikiana na Shirika la Posta Tanzania imejidhatiti kutoa huduma kwa wahitaji na wananchi ambao wamekuwa wakienda masafa marefu kutafuta huduma.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dodoma na Seif Suleiman Mohammed meneja wa tawi la PBZ Dar es salaam pia ni msimaizi wa mafunzo ya huduma za benki kwa mawakala wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na adhima ya benki hiyo katika kuimarisha huduma zake.
Meneja huyo alifafanua kuwa katika kuhakikisha huduma za kibenki zinaimarishwa kwa wananchi wote hapa nchini wamenza kutoa mafunzo ya namna benki ya watu wa Zanzibar wanavyofanya kazi.
“Mafunzo haya yanatolewa hapa dodoma kwa maafisa mbalimbali kutoka mikoa tofauti ili kuweza kuboresha utoaji wa huduma za benki hiyo kwa wananchi,”alisema.
Alisema kuwa hii ni kutikana na kwamba Dodoma ni makao makuu na pia ni katikati ya nchi, hivyo benki ya watu wa Zanzibar imedhamiria kutoa huduma.
Wananchi wamekuwa wakitumia masafa marefu ili kutafuta huduma na kuwafanya wapoteze muda mwingi na gharama.
Kwa upande wake Rehema Mbunda meneja wa huduma za fedha na uwakala shirika la posta makao makuu Dar es salaam, alisema kuwa Benki ya watu wa Zanzibar imeamua kuingia ubia na shirika la posta Tanzania kwa sababu tayari kwa bara kuna matawi 360 na wanatoa huduma hivyo wananchi wengi zaidi watanufaika na ubia huo.
“Wananchi watarajie kupata huduma nzuri sababu posta imetapakaa katika sehemu nyingi na sasa benki ya watu wa zanzibar imejidhatiti kuwafata wananchi mpaka vijijini ili kuwapatia huduma,”alisema Rehema.
Alisema kuwa Benki ya watu wa Zanzibar imeona ni bora ikatoa mafunzo kwa Maafisa kutoka mikoa tofauti tofauti ili kuweza kutoa huduma za kibenki kwa wananchi.