NA NASRA MANZI

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Riziki Pembe Juma amewataka walimu wa Unguja na Pemba,  kuendelea kushirikiana katika kuibua vipaji vya sanaa na michezo kwenye ngazi za skuli zao.

Akizungumza katika usiku wa Sanaa ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za tamasha la elimu bila malipo,iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa AbdulWakil Kikwajuni.

Alisema jambo hilo litasaidia kupatikana wanamichezo na wasanii ambao, wataitangaza Zanzibar kupitia sanaa  pamoja na michezo mbali mbali.

Hata hivyo alisema walimu wamekuwa wakifanya juhudi kubwa kuibua vipaji kwa wanafunzi wao,lakini ni vyema kuendelea kutumia busara katika ufundishaji,jambo ambalo  litasaidia kuibua vipaji vingi zaidi.

Alisema Wizara na Idara zimekuwa mstari wa mbele kuibua  vipaji na kuvilea kuanzia ngazi za misingi na baadaye kuendelezwa hadi sekondari.

Katibu Mkuu Wizara  hiyo Idrissa Muslih Hija aliwapongeza walimu kwa kuwafundisha sanaa na michezo wanafunzi na kufikiwa kiwango kizuri.

Mkurugenzi Idara ya Michezo na Utamaduni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Hassan Khairalla Tawakal, alisema Idara itaendelea kuhuwisha na kufufua shughuli za michezo na sanaa zenye mnasaba wa kuitangaza nchi.