MILAN, Italia
KIUNGO mshambuliaji wa kimataifa wa Croatia, Ivan Perisic, amerejea Inter Milan akitokea kwa mabingwa wa Ulaya, Bayern Munich alipokua anatumika kwa mkopo.

Meneja wa Bayern, Hansi Flick amethibitisha kuondoka kwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 31, baada ya kutumika klabuni hapo kwa msimu 2019–2020.

Perisic aliondoka Inter Milan kwa mkopo wa euro milioni tano huku, Munich wakipewa sharti la kumnunua kwa euro milioni 20, endapo wangelivutiwa na kiwango chake.

Hata hivyo mpango wa kiungo huyo kusajiliwa moja kwa moja kwa mabingwa hao wa Ujerumani ulishindikana, baada ya mazungumzo ya pande hizo mbili kugonga mwamba, hasa kwenye kipengele cha kushushwa kwa ada yake ya usajili.

Mbali na Perisic, Flick amethhibitisha kuondoka kwa wachezaji wengine kama Alvaro Odriozola aliyerejea kwa mabingwa wa Hispania, Real Madrid na Philippe Coutinho aliyerudi Barcelona.

Perisic amecheza michezo 35 na kufunga mabao manane akiwa na Bayern Munich na kuchangia kutetea taji la Bundesliga na kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.(Goal).