LONDON, England

KIUNGO wa Manchester United, Paul Pogba amerejea katika mazoezi ya kikosi hicho baada ya kuwa nje, lakini kuna uwezekano mkubwa wa kutocheza mchezo wa awali dhidi ya Crystal Palace.

 Manchester United itavaana na Crystal Palace, Septemba 19, mwaka huu kwenye Uwanja wa Old Trafford ikiwa ni mchezo wa kwanza msimu huu ndani ya ligi kuu.

Pogba hakuwa sehemu ya kikosi hicho ambacho kilikuwa kinaendelea na mazoezi na hii ni kutokana na kupata maambukizi ya Virusi vya Corona.

Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amesema, Pogba amerejea kwenye mazoezi lakini hajawa imara kwa asilimia 100 katika mechi ijayo hana uhakika kwenye hilo.

Solskjaer amesema: “Paul alifanya mazoezi ya awali, lakini baadaye akawa nje kutokana na kupata Virusi vya Corona hivyo akawa nje ya timu.

“Ninaamini atakuwa imara tena kwa haraka sababu alianza kufanya mazoezi binafsi kwa bidii akitokea karantini na sasa amejiunga na timu’’.

“Matumaini yangu ni kuona wiki ijayo anakuwa mzima kwa ajili ya kupambana ingawa kwenye hilo sina uhakika, kwani anaweza kukosa mchezo wa kwanza,”