NA SAIDA ISSA, DODOMA

KATIBU wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Hamphrey Polepole, amewataka wagombea waliothibitishwa na chama hicho kuwania ujumbe wa baraza la wawakilishi kujaza fomu za uteuzi kwa umakini ili kuepuka kuwekewa pingamizi.

Akizungumza na wanahabari jijini Dodoma wakati akitangaza majina ya wanachama wa chama hicho kugombea nafasi hizo baada ya kikao cha kamati kuu kilichofanya uteuzi huo kwa niaba ya halmashauri kuu ya CCM Taifa.

Alisema ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa usahihi, chama hicho kimeandaa wanasheria Zaidi ya 70 ambao watashirikiana na wateule hao ili kuepusha ukiukwaji wa taratibu.

“Tumefanya hivyo ili tutakaporudisha fomu hizo kule Zanzibar, hakuna mtu ambaye atathubutu kuweka pingamizi,” alisema polepole.

Aidha aliwaasa wanasiasa wa vyama vya siasa kuacha kutoa lugha chafu na kuwasema viongozi wa chama hicho katika kampeni zao badala yake watoe hoja za msingi zitakazokuwa na maslahi kwa Watanzania.

“Kuna baadhi ya wagombea badala ya kunadi sera na ilani zao, wamejipa kazi ya kuwasema viongozi wetu na chama chetu. Kazi ya kukisemea chama ni yetu sisi wao waeleze wanataka kuwafanyia nini watanzania japo tunajua kuwa hawana hoja,” alisema Polepole.

Akizungumzia uteuzi huo, alisema kamati kuu ya halmashauri kuu, imefanya uteuzi wa mwisho wa wanachama wake walioomba kugombea nafasi ya ujumbe wa Baraza la wawakilishi Zanzibar ili kupata viongozi watakaomsaidia Dk. Hussein ali mwinyi katika serikali atakayoiunda iwapo atapewa ridhaa ya kuiongoza Zanzibar.

“Zanzibar inataka wawakilishi wanaotambua changamoto za wananchi na watakaotambua fursa na kuzitumia kwa maslahi ya Zanzibar ikiwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alieleza Polepole.