NA MWANAJUMA MMANGA

JESHI la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, limesema litahakikisha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 ya mwaka huu unafanyika kwa amani, usalama utulivu wa hali ya juu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Suleiman Hassan Suleiman, aliyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili huko ofisini kwake Tunguu Wilaya ya Kati, Unguja.

Alisema iwapo amani itatawala kutaweza kupatikana maendeleo makubwa kwa wananchi wake na jeshi hilo limejipanga kuanzia katika hatua za maandalizi ya uchaguzi na kwamba watahakikisha wanasimamia usalama wa raia na mali zao.

Alisema Oktoba 27 na 28 mwaka huu siku ambazo uchaguzi utafanyika kwa kura ya mapema, kutakuwa na harakati nyingi za uchaguzi wa kumchagua Rais wa Tanzania na wa Zanzibar, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani

“Tunafahamu kuwa kuelekea uchaguzi huu kutakuwa na mikutano ya kampeni itafanyika katika maeneo mbalimbali ya mkoa wetu hivyo kama taasisi yenye dhamana ya ulinzi tutahakikisha mikutano hiyo inafanyika kwa usalama wa hali ya juu,” aliongeza Kamanda Suleiman.

Alifafanua kuwa watahakiisha wanasimamia usalama wa barabrani na kuwaomba wananchi na viongozi wa vyama vya siasa kuhakikisha wanatii sheria bila ya kushurutishwa kwa usalama wao.

Alisema katika mkoa huo kutakuwa na askari wao wa operesheni barabarani watakaohakikisha usalama unakuwepo muda wote, lakini pia katika hatua zote za uchaguzi huo.

Aidha aliwashauri viongozi wa vyama vya siasa kufuata kikamilifu ratiba zao na kama kutakuwa na jambo linahitaji muongozo wa tume ya uchaguzi, wafanye mawasilino mapema ili kuepusha changamoto bila ya vurugu.