NA ASIA MWALIM

JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja linamtafuta dereva wa gari aliesababisha kifo cha mpanda pikipiki Sabri Khamis Sumri (55) mkaazi wa Kariakoo wilaya ya Mjini, mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Kamanda wa Polisi mkoa huo Kamishna Msaidizi (ACP) Awadh Juma Haji alithibitisha kutokea kwa tukio hilo wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake Mwembemadema.

Alisema dereva huyo aligonga na kusababisha kifo hicho alipokua akiendesha gari ambayo haikua na namba za usajili, na hajafahamika jina lake wala mmiliki halali wa gari hilo.

Alieleza kuwa baada ya tukio hilo mtuhumiwa alikimbia na hajulikani mahali alipo hata hivyo jeshi hilo linaendelea kumsaka muhalifu huyo.

Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 8, mwaka huu majira ya saa 1:30 usiku huko barabara ya Mwera maeneo ya Mtofaani kwa kijambia ambapo gari hilo liliweza kumgonga mpanda pikipiki yenye namba za usajili Z. 918 KZ aina ya ‘Today’ rangi ya silver aliekua akitokea upande wa Masingini kuelekea Mwera.

Aidha Kamanda alieleza kuwa mpanda pikipiki baada ya kugongwa alipata majeraha sehemu ya kichwa yaliyoweza kusababisha kifo chake huko hospitali kuu ya Mnazi Mmoja wakati akipatiwa matibabu hospitalini hapo.   Kamanda Awadh alisema chanzo cha tukio hilo ni mwendo kasi ulio sababishwa na dereva wa gari, hivyo Jeshi hilo linaendelea kumtafuta mtuhumiwa huyo baada ya kupatikana atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.