NA HUSNA SHEHA

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Haji Abdalla Haji, amevipongeza vyama vya siasa kuendesha kampeni zao kwa kufuata masharti na misingi iliyowekwa na jeshi hilo.

Akizungumza na Zanzibar Leo huko Ofisini kwake Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja, alisema tangu kuanza kwa kampeni katika mkoa huo hakuna tukio lolote la kihalifu lilojitokeza linalotokana na vyama vya siasa au wafuasi wao.

Alisema changamoto kubwa katika gari ambazo zinapakia kupita kiwango hali ambayo inaweza kusababisha ajali zisizokuwa za lazima.

Kamanda Haji, alisema katika kuona hali inaondoka Jeshi la Polisi limekuwa likichukua jitihada za kudhibiti hali hiyo na kuona madereva wanapakia watu kwa idadi ya gari zao.

“Hali hii tumeanza kuidhibiti mapema endapo tukiona watu wamejazwa katika gari basi tunachukua hatua ya kuwashusha kwani hatutaki kuona wananchi wanapoteza maisha yao nasi ndio tuliopewa jukumu la kulinda raia na mali zao,” alisema.

Aidha alisema kabla ya kuanza kampeni viongozi wa vyama vya siasa walifanya mazungumzo kuona wafuasi wao wanatii sheria za barabarani.

Hivyo alibainisha kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika kipindi chote cha kampeni, ili kuona wananchi wanaenda katika mikutano kwa salama na amani.

Mbali na hayo aliwashauri wananchi wanaokwenda mikutanoni kuacha mihemko ya kutumia lugha ambazo zitasababisha kuleta mifarakano na badala yake kutumia lugha za kistaarabu.

 Sambamba na hayo aliwasisitiza kuacha kubandika picha za wagombea wao katika maeneo yasioruhusiwa, ili kujiepusha na matatizo yasiyokuwa ya lazima.

“Kuna baadhi ya watu wanabandika picha za wagombea katika maeneo bila ya ridhaa ya wahusika, ile inasababisha uchochezi sio vizuri,” alisisitiza.