NA LAILA KEIS
JESHI la Polisi limetoa onyo kwa wanaovunja sheria za usalama barabarani kwa makusudi, wakati wa kwenda na kurudi katika mikutano ya kisiasa inayoendelea.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Awadhi Juma Haji, aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Mwembemadema mjini Unguja.
Alisema, ndani ya Mkoa huo, kumeibuka tabia kwa baadhi ya waendao mikutanoni kupakia abiria kwa njia ya hatari, kujaza abiria kupita uwezo wa gari, kuendesha kwa mwendo kasi, abiria kucheza ngoma wakiwa ndani ya gari huku gari hilo likiwa katika mwendo kasi.
Pia alisema, baadhi yao hutumia vyombo vya maringi mawili kubeba abiria zaidi ya mmoja, na kuendesha kwa mbwembwe zinazohatarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara.
Sambamba na hilo alisema, pia kumeibuka tabia ya kufunika namba za usajili wa magari na vyombo vya maringi mawili kwa kuweka stika za bendera za vyama, zinazoficha namba za usajili wa vyombo vyao.
Alisema, kitendo hicho kitapelekea kutoa mwanya kwa wahalifu, ambao watafanya hivyo kwa lengo la kuficha wasikamatwe kirahisi pindi watakapofanya uhalifu au kusababisha ajali za barabarani na kukimbia.
Alisema, wanaofanya vitendo hivyo hufanya kwa utashi wao wenyeweye, kwani viongozi wa vyama vyao hawawaamuru kufanya hivyo.
Hivyo, Jeshi la Polisi la Mkoa huo linatoa onyo kali na kuwataka waache mara moja vitendo hivyo, kwani halitoruhusu vitendo vya ukiukwaji wa sheria, na hatua kali ya kisheria itachukuliwa kwa yeyote atakaebainika kufanya vitendo hivyo.
Kwa hatua nyengine, aliwataka wagombea kufanya kampeni za kistaarabu, huku wakitanguliza maslahi ya nchi kwa kuhubiri amani katika kampeni zao, ili amani iendelee kudumu nchini.